NEWS ROUND 30 APRIL 2014.


DODOMA
Wananchi na Viongozi wa vyama vya siasa  Manispaa ya Dodoma wameelezea mitazamo yao Mara baada ya bunge maalumu la katiba kusitishwa kuhusu upatikanaji wa katiba bora. 
Akizungumza na kituo hiki Mjasiria mali ambaye ni fundi wa kushona nguo Bwana Kharid zoya amesema kwa mujibu wa taratibu za bunge maalumu ana imani kuwa katiba mpya itapatikana  na kwa wakati.
Naye  Afisa Idara ya Mipango na mikakati wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Bwana Emannuel Suday amesema mchakato  wa katiba mpya ulitekwa tangu awali na chama Tawala katika mabaraza ya katiba.
Kwa upande wake katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini Bwana Kanuthi Ndegine amekanusha juu ya malalamiko yanayotolewa na vyama vya siasa na wananchi kuwa katiba itakayotengenezwa itakuwa yenye mlengo wa Chama tawala.
Sanjari na hayo Mjumbe wa bunge maalumu la katiba anayetoka ktika kundi la watu 201 BI Magdalena Rwebangira amesema kilichofanyika kwa siku hizo 67 ni  kupata maoni ya wajumbe kuhusiana na sura ya kwanza na ya sita.
-------------------------------------------------------------------------------------------
Takwimu zinaonyesha  ugonjwa  wa malaria unawashambulia zaidi watoto wenye  umri chini ya wa miaka mitano kutokana na wazazi kutojua matumizi  sahihi ya vyandarua.
Wakizungumza na kituo hiki baadhi ya wazazi katika manispaa ya Dodoma wamesema wamekuwa wakipewa elimu ya matumizi sahihi ya vyandarua katika kliniki mbalimbali lakini baadhi ya akina mama hawazingatii mafunzo hayo.
Nae Bi, Kishe mkazi wa majengo amesema ni vema wazazi wenye watoto chini ya umri wa  miaka mitano wawahishe watoto  hospitali mapema mara tu wanapoona mtoto ana dalili za malaria.
Akitoa Takwimu za ugonjwa wa Malaria kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano  mratibu wa malaria kwa Mkoa wa Dodoma Dr Fransisco Bujiku amesema  takwimu za mwaka 2012 zinaonyesha watoto ambao hawajaugua malaria ni  lakimoja na sabini na moja walio ugua malaria ni  miatatu sabini na moja ambayo ni asilimia 391%.
---------------------------------------------------------------------------------------------
Wakulima mkoani Dodoma wametakiwa  kujihusisha na kilimo cha uyoga kwani zao hilo ni  stahimilivu kwa mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumza na kituo hiki muelimishaji na mkulima wa zao hilo ndugu Emanuely steven toka msalato amesema kuwa  zao la uyoga ni ufumbuzi wa mabadiliko ya tabia nchi kwani si tegemezi kwa mawingu na halina msimu.
Aidha mtaalamu huyo  amewaasa wakulima  kuto kulima kilimo cha mazoea bali watafute njia mbadala zitakazo wawezesha kuendelea kulima mazao yanayo kabiliana na mabadiliko ya tabia Nchi.
Naye bi Diana Bwahama  mkazi wa Area A ambaye pia ni mkulima wa uyoga  amesema mbinu wanazo tumia ili kufanikisha  kilimo cha Uyoga   ni kufuata taratibu wanazo pewa na wataalamu wa kilimo hicho.
Uyoga hustawi vizuri kwenye maeneo yenye joto la wastani wa nyuzi joto 20 hadi 33 na unyevu wa kiasi cha asilimia 75 hivyo kuwa rafiki kwa mazingira ya mkoa wa dodoma.
KITAIFA
Watu 19 wakiwamo askari polisi wanne wa Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Singida wamekufa papo hapo baada ya kugogwa na basi la Sumry lililokuwa linatoka Kigoma kwenda Dar es Salaam.
Watu hao pamoja na wanakijiji wenzao, wakiwamo sita waliojeruhiwa, walikuwa wamekusanyika kando ya barabara kushuhudia ajali iliyotokea awali, ambayo mwendesha baiskeli alikuwa amegongwa na lori na kufariki dunia papo hapo. Katika mkusanyiko huo, ndipo basi hilo lilipowapitia na kukatisha maisha yao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Joseph Malunda amesema miili ya marehemu iliyofikishwa katika hospitali hiyo ilikuwa imeharibika vibaya, baadhi ilikatika viungo mbalimbali kama shingo, miguu, mikono na nyingine utumbo na ubongo ulimwagika nje.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela amesema baada ya basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Paul Njilo mkazi wa Dar es Salaam kukanyaga watu hao, halikusimama hapohapo, badala yake alikimbia na kwenda kulitelekeza baada ya kilomita 25 katika Stendi Kuu ya Utaho na kukimbilia kusikojulikana.
----------------------------------------------------------------------------------------------------------
KIMATAIFA .
Kamishna mkuu wa haki za binadamu kutoka  Umoja wa Mataifa Bibi Navi Pillay amelaani  vikali hukumu ya kifo iliyotolewa kwa wafuasi 683 wa Chama cha Muslim Brotherhood nchini Misri. 

Taarifa hiyo inakuja siku moja baada ya watu hao kuhukumiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo kumwua polisi mmoja na kuvamia kituo cha polisi cha Edwa huko Al-Minya tarehe 14 Agosti mwaka jana.

 Taarifa hiyo imesema, ndani ya miezi miwili hukumu mbili za kikatili kama hiyo zimetolewa na mahakama ya makosa ya jinai mjini Al-Minya. Tarehe 24 Machi, ambapo watu 529 walihukumiwa adhabu ya kifo.

Bibi Pillay ameongeza kuwa, ni lazima Misri itekeleze ahadi zake mara moja kuhusu haki za binadamu kwa kufuata Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa.

---------------------------------------------------------------------------------------------------
Wapiga kura nchini Iraq wanashiriki katika zoezi la upigaji kura katika mikoa yote isipokuwa mkoa mmoja katika uchaguzi wa kwanza wa wabunge tangu wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo mwaka 2011.
Waziri mkuu wa sasa Nouri al-Maliki anagombea kiti chake kwa muhula wa tatu lakini kampeni zimekuwa zikipigwa kwa misingi ya vurugu za kisiasa zinazoendelea kukithiri nchini humo.
Selikali ya muungano ya bwana Maliki inayoongozwa na chama cha Kishia imekabiliwa na wakati mgumu kupambana na uasi unaongozwa na kundi lenye ufungamano na Al Qaeda katika mji wa Falluja na mkoa wa Anbar.
Helikopta za kijeshi zinashika doria katika anga ya Baghdad na serikali imefunga uwanja wa ndege na baadhi ya barabara kuu ndani na nje ya mji huo.

Comments