HAKUNA TENA KUNUNUA VX: RAIS HICHILEMA

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amewataka Watumishi wa Serikali wanaotaka wapewe magari ya kifahari aina ya Toyota Land Cruiser VX kwa ajili ya kuyatumia kwenye kazi wasau hilo na kama wanaona yana umuhimu sana basi wajinunulie wao lakini sio kwa pesa za Serikali.

Hichilema amehoji “Kwanini mnatumia pesa kumnunulia Meya VX? hiyo pesa ya kumnunulia Meya VX inaweza kuweka vyoo katika masoko yote kwenye miji yenu, piteni katika mstari huo.... Meya bado anaweza kuendesha gari zuri kama vile Hilux double cabin sio lazima gari liwe VX, mkitaka kuendesha VX nunueni kwa pesa zenu”

Kwa upande mwingine Rais huyu ambaye hakutaka kupokea mshahara wa Urais kwa miezi nane akisema kilichomsukuma kuingia madarakani sio pesa bali uzalendo wa kuijenga Nchi yake, aliwataka pia Watumishi wa Serikali wanaotaka kuongezewa mishahara wafikirie Wananchi ambao wanateseka kabla ya kutaka nyongeza hiyo "Unapoona mshahara unaingia kwenye akaunti yako ya benki kumbuka ni Mama Mjane amenilipa mshahara huu kwa hiyo kabla ya kuomba nyongeza jiulize vipi kuhusu yule anayekulipa mshahara wako wa sasa? Mtoto wake anakaa chini darasani.” Rais Hakainde Hichilema

Comments