Shule yaboreshewa huduma za Tehama

SHULE ya Sekondari Nyumbu, Kibaha mkoani Pwani, imeboreshewa chumba cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa kupewa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 17, vikiwemo vishikwambi 15.

Msaada huo umetolewa na Taasisi ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na Helios Towers kwa lengo la kusaidia wananchi wakiwemo wanafunzi kupata huduma ya mtandao wa kidijiti iwasaidie kupata maarifa zaidi ya kielimu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo shuleni hapo, Mjumbe wa Bodi ya Taasisi Vodacom Tanzania, Olaf Mumburi alisema dhamira ya taasisi hiyo ni kuunganisha kila mwananchi katika mtandao wa kidijiti.

Alisema vifaa hivyo vitasaidia wanafunzi kupata manufaa ya elimu kwa kuongeza maarifa kupitia matumizi sahihi ya mtandao.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vishikwambi 15, vipakanjia vitatu, televisheni moja, printa moja na kifurushi cha data cha mwaka mmoja vyenye jumla ya Sh milioni 17.

Alisema Vodacom Tanzania Foundation imekuwa ikitoa vifaa vya Tehama shuleni tangu mwaka 2016 kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni Samsung, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), African Child Projects, Mamlaka ya Elimu Tanzania na Helios Towers.

Hadi sasa wametoa misaada yenye thamani ya takribani Sh milioni 700 kwa shule zaidi ya 500 nchini kupitia programu ya e-Fahamu.

“Leo hii tunashirikiana na kampuni ya Helios Towers na ushirika wetu utawanufaisha wanafunzi wa Sekondari ya Nyumbui kupata elimu ya Tehama itakayowawezesha kunufaika na mageuzi ya kidijitali na kushiriki katika ulimwengu wa utandawazi,” alisema Mumburi.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri alisema serikali imedhamiria kuendelea kuimarisha ubora wa elimu na kuhakikisha inaendana na ukuaji wa mageuzi ya kidijiti ili kuhakikisha elimu inayotolewa katika ngazi zote inaleta maendeleo ya uchumi na jamii nchini.

Comments