TANZANIA na Msumbiji zimekubaliana kuongeza kiwango cha uwekezaji na biashara ili kuimarisha uchumi na ustawi wa watu wa nchi hizo mbili.
Hayo yamebainishwa na Rais Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji kwenye mkutano wao na vyombo vya habari mjini Maputo Jumatano.
Rais Samia alisema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Msumbiji kimeshuka kutoka Sh bilioni 53 hadi kufikia Sh bilioni 26 katika kipindi cha mwaka huu, hivyo wanahitaji kulifanyia kazi eneo hilo muhimu.
“Tumekubaliana kwamba tutumie fursa za kibiashara na uwekezaji hasa katika eneo la kilimo, uvuvi na uchimbaji madini,” alisema Rais Samia.
Kuhusu hoja hiyo ya uwekezaji na biashara, Rais Nyusi alisema Msumbiji imekuwa katika mdororo wa uchumi kutokana na kupitia wakati mgumu ikiwamo mabadiliko ya hali ya hewa na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine iliyopunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha biashara.
“Ziara hii ya Rais Samia itasaidia kuimarisha uhusiano wetu wa kibiashara na kuinua kiwango cha uchumi na uwekezaji. Tulikuwa na maonesho ya biashara hapa Msumbiji na Watanzania walileta bidhaa zao,” alisema Rais Nyusi.
Pia Rais Samia alisema wamezungumza kuhusu umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana katika kufanya biashara baina yao kwa kuwa nchi hizo zimekuwa zikifanya biashara zaidi na watu nje hasa nchi za Asia na Ulaya.
Alisema ili kuondokana na changamoto hiyo, wamekubaliana namna ya nchi zao zitafanya biashara pamoja na endapo watafanikiwa kufanya biashara baina yao, watakuwa wameweka msingi wa biashara.
Alisema anatambua kampuni za Tanzania zilizopo nchini Msumbiji lakini hazitoshi, hivyo kuna haja ya kuongeza kiwango cha uwekezaji kutoka pande zote mbili.
“Katika kutumia rasilimali zetu za gesi, tumekuwa tukiwashirikisha wadau wa nje wenye uzoefu zaidi katika uchimbaji wa gesi na mafuta, kwa hiyo tunaweza kushirikishana uzoefu, kujifunza kutoka pande zote mbili na kulinda rasilimali zetu,” alisema Rais Samia.
Eneo jingine ambalo marais hao walikubaliana kuendelea kushirikiana na la ulinzi na usalama ikiwamo eneo la mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji.
Katika hilo, Rais Samia alisema kuna haja kwa nchi zao kuendelea kudumisha amani na utulivu na kupambana na ugaidi na kitisho kingine chochote cha ulinzi na usalama.
Alisema kutokana na umuhimu huo, Tanzania na Msumbiji zilitiliana saini katika eneo la ulinzi na usalama pamoja na eneo la utafutaji na uokoaji.
Kuhusu ulinzi na usalama, Rais Nyusi alisema mbali na kupambana na ugaidi, pia Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kupambana na biashara ya dawa za kulevya na biashara ya binadamu.
Pia viongozi hao walikubaliana Lugha ya Kiswahili ianze kufundishwa Msumbiji ili kurahisisha mawasiliano kati ya watu wa nchi hizo mbili.
Maeneo mengine waliyokubaliana ni kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii, kubadilishana wanafunzi wa elimu ya juu ili vijana wa Tanzania na Msumbiji waishi pamoja kama ndugu.
Rais Samia yupo nchini Msumbiji kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia juzi mpaka leo.
Comments
Post a Comment