Katavi waja kivingine, kilimo, utalii

MKOA wa Katavi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na utalii, imeandaa maadhimisho ya wiki ya mwana Katavi itakayoanza Oktoba 22, 2022 hadi Novemba 2, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, leo Oktoba 17, 2022, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amesema maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali za kilimo, pamoja na bidhaa za viwandani.

Amesema lengo la maonesho hayo ni kutoa elimu ya kilimo bora na cha kisasa, pamoja na kutoa hamasa kwa wananchi kufanya kilimo cha kisasa na kutangaza fursa mbalimbali mkoani Katavi.

Ameeleza kuwa maonesho hayo yataambatana na shughuli ya ugawaji wa mbolea ya ruzuku kwa wananchi, ikiwa ni uzinduzi wa msimu wa kilimo, kama maandalizi ya kuelekea msimu huo.

Ameongeza, katika wiki hiyo ya mwana Katavi litaanza tukio la Miss Utalii, Oktoba 22,  ambapo kutakuwa na mashindano ya kumsaka Miss Utalii ndani ya Mkoa wa Katavi.

Pia amesema kutakuwa na tukio la kutembelea mbuga ya wanyama ya Katavi kwa ajili ya kujionea vivutio mbalimbali ndani ya mkoa huo.

Chanz0: Habari Leo

Comments