Ruto: Mabishano ya Tanzania na Kenya tumeyaweka nyuma

Rais wa Kenya, William Ruto amesema yale mabishano yaliyokuwepo baina ya Tanzania na Kenya wameyaweka nyuma.

Rais Ruto ameyasema hayo leo Oktoba 10, 2022 wakati akizungumza Ikulu Dar es Salaam akitaja baadhi ya mambo waliyokubaliana na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha biashara na kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo.

“Ile historia ya zamani kidogo mabishano tumeyaweka nyuma yetu, tunataka kujenga mahusiano mema, tunataka Watanzania wafaidike na tunataka Wakenya wafaidike, Wakenya wakifaidika na sisi, Tanzania itafaidika,”ameeleza.


Rais Ruto amesema wanataka kujenga uchumi wa pamoja na kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na yapo mengi watayafanya wakiwa pamoja.

“Rais atahesabu ushirikiano wangu, Serikali yangu ipo tayari kufanya kazi kwa maslahi ya nchi zetu mbili,”amebainisha.

Pamoja na hayo Rais Ruto amebainisha kwamba Tanzania na Kenya wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kudhibiti vitendo vya ugaidi na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

“Tumekubaliana vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kushirikiana kuangalia makosa yanayovuka mipaka, madawa ya kulevya, uharamia, ujangili na usafirshaji wa watu,”amesema Rais Samia

Rais Samia amesema Tanzania na Kenya zinapata taswira mbaya ya usafirishaji wa binadamu.

Amesema kinachofanyika ni kuwakamata wahalifu pekee lakini kwenye rekodi za dunia taswira inakuwa mbaya, kuna haja kuchukuliwa hatua kudhibiti zaidi bishara hiyo.

Chanzo: Mwananchi

Comments