Vikwazo 14 biashara Tanzania, Kenya kuondolewa

Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya, William Ruto wametoa maagizo kwa mawaziri wa Uwekezaji kuhakikisha wanaondoa vikwazo 14 vya biashara baina ya nchi hizo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 10, 2022 Ikulu Dar es Salaam ikiwa ni miongoni mwa mambo waliyojadiliana kutafutiwa ufumbuzi wa haraka kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Kazi hii ilianza na Rais Mstaafu, Uhuru Kenyata na tulikubaliana kwa kuwataka wataalamu wetu kufanyia kazi vikwazo vya biashara vilipo.


“Mawaziri hao walitambua vikwazo 68 na vilifanyiwa kazi 54 na tumewataka sasa mawaziri wetu wakutane na kufanyia kazi vikwazo hivyo ili kuwe na uhuru wa kibiashara” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema ziara ya Ruto inatoa fursa ya kutathimini fursa ya ushirikiano katika ngazi zote

 “Tanzania na Kenya tusigawane umasikini na udhalili lakini tugawane utajiri tutakaofanya kupitia biashara,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Rais wa Kenya, Willam Ruto amesema Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania akibainisha kwamba, kuondoshwa kwa changamoto hizo kumeinufaisha zaidi Tanzania ikilinganishwa na Kenya.

Amesema biashara baina ya Tanzania na Kenya imezidi kuimarika ambapo usafirishaji wa bidha kwa mwaka mmoja imepanda kutoka Sh27 bilioni kutoka Tanzania kufikia Sh50 bilioni kwenda Kenya.

Kwa upande wa Kenya amesema usafirishaji wa bidhaa kutoka Kenya kuja Tanzania imepanda kutoka Sh31 bilioni kufikia Sh45 bilioni.

“Leo tunanunua vitu vingi kutoka Tanzania kuliko wanavyonunua kutoka Kenya na hii ni kutokana na ushirikiano baina ya nchi zetu.”ameeleza

Rais Ruto amesema Mawaziri baina ya Kenya na Tanzania wanapaswa kufanyia kazi changamoto zilizobaki na kufikia mwishoni mwa mwaka huu changamoto zote zimetatuliwa.


Rais Ruto yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo aliwasili jana na leo kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kufanya mazungumzo Ikulu, Dar es Salaam.


Chanzo: Mwananchi

Comments