Tanzania yaanza mchakato kujenga satelaiti

Serikali imesema katika mwaka huu wa fedha imeanza kuandaa utaratibu wa kuunda na kurusha satelaiti yake angani.

Akizungumza bungeni leo, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo amesema Serikali imeunda andiko dhana na timu ya watalaamu watakaoshauri aina ya satelaiti itakayorushwa angani.

Naibu Waziri Mathew Kundo amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza programu ya kuunda na kurusha setelaiti angani.

“Ni matarajio kuwa timu hiyo itakamilisha kazi ya uchambuzi na kuwasilisha mapendekezo yake Serikalini kwa hatua za kimaamuzi ndani ya mwaka huu wa fedha,” amesema Kundo.

Naibu waziri amezungumzia satelaiti zilizopo Afrika ambapo amesema hadi sasa Afrika ina jumla ya satelaiti 41, na kuanzia mwaka 2016 ni satelaiti 20 tu ambazo zimekuwa angani.

Comments