Uingereza, Tanzania kufanya kongamano la kibiashara

UBALOZI wa Uingereza na Serikali ya Tanzania wanatarajia kufanya kongamano la pili la kibiashara kutambua fulsa za kibiashara na uwekezaji utakaosaidia kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kongamano hilo leo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ally Gugu alisema kongamano hilo litafanyika Novemba 29, 2022 Dar es Salaam na kuwaleta pamoja wafanyabiashara zaidi ya 100 kutoka katika nchi hizo.

Alisema wafanyabiashara hao watatambua fulsa za biashara na uwekezaji katika kubadilishana maarifa juu ya kufanya biashara nchini ambapo ni fulsa kwa Tanzania kuongeza mauzo ya nje ya nchi kwenda Uingereza.

“Kwa kuzingatia ahadi kutoka katika kongamano la mwaka jana, kwa mwaka huu tutajumuisha vikao kadhaa vya kupeana taarifa na mijadala…

…pia kutakuwa na jopo inayohusisha wataalam wa biashara na uwekezaji, kusaidia kuboresha mazungumzo kati ya serikali na sekta binafsi ili kuongeza imani ya wawezaji na biashara” alisema

Gugu aliwataja watakaoongoza kongamano hilo kuwa ni Mjumbe wa Waziri Mkuu wa Uingereza wa biashara nchini Tanzania, Lord Walney na Waziri wa nchi, Ofisi ya rais, kazi, uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mudrik Ramadhani Soranga

Aliongeza kwa kusema kutakuwa na Naibu kamishna wa biashara wa Afrika , Alistair Long na ujumbe wa wafanyabiashara zaidi ya 24 wa Uingereza kutafuta fulsa na kuimarisha uhusiano.

Alisema kutasainiwa mpango kazi wa pamoja na hotuba za mawaziri wa uwekezaji wa biashara kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

Mjumbe wa Waziri Mkuu Walney naye alisema amefurahi kurejea Tanzania, akileta kundi la wafanyabiashara wa Uingereza ili kuimarisha zaidi biashara na uwekezaji na kuleta ustawi pande zote.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kusaidia wawekezaji na wafanyabiashara kama waliopo hapa leo, wanaochangia uwezo watanzania kiuchumi” alisema.


Source: Habari Leo

#uk #unitedkingdom #tz #tanzania

Comments