Biden aapa kuimarisha msaada kwa Ukraine

Rais Joe Biden wa Marekani ameapa kuongeza msaada kwa Ukraine alipomkaribisha rais Volodymyr Zelensky katika ikulu ya Washington jana Jumatano huku akiahidi kuendelea kuimarisha uwezo wa Ukraine wa kujilinda.

Rais Joe Biden wa Marekani amemwambia Volodymyr Zelenskyy kwamba Kyiv haitabaki peke yake, kwenye vita hivyo ingawa aliweka wazi kwamba kutakuwa na ukomo wa misaada itakayoendelea kupelekwa nchini Ukraine, ambayo mwisho wa siku haitaleta mgawanyiko miongoni mwa washirika wake.

Zelenzkyy ambaye yuko Marekani katika ziara ya kwanza ya nje ya nchi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi Februari, kwa upande wake amesema hatakubali kushinikizwa kuingia kwenye mapatano ya amani yatakayoyaweka rehani maeneo ya Ukraine, ambayo miongoni mwake Urusi inadai ni ya kwake.

Amesema vita nchini mwake vitaisha wakati Ukraine itakapokuwa huru, pamoja na kulipwa fidia kufuatia uharibifu uliofanywa wakati wa uvamizi wa Urusi.

Kiongozi huyo wa Ukraine aidha ameishukuru Washington kwa kukubali kuwapa mfumo wa kisasa wa kujilinda na makombora angani wa Patriot ambao ni sehemu ya msaada wa kijeshi wa mabilioni ya dola uliotangazwa wakati wa ziara yake. Amesema, mfumo huo utawasaidia pakubwa kuimarisha ulinzi wa angani na kuongeza kuwa ni hatua muhimu katika kuandaa anga salama kwa Ukraine.

Biden awali, alimshutumu rais wa Urusi Vladimir Putin, akisema haonyeshi nia yoyote ya kumaliza vita dhidi ya Ukraine na kuongeza kuwa inaumiza kwa kile anachokifanya Putin cha kushambulia shule na vituo vya watoto yatima nchini Ukraine, huku kwa upande mwingine akimsifu Zelenskyy kwa utayari wake wa kufanya mazungumzo ya kusaka amani.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, Biden alionya kwamba Urusi inajaribu kuyatumia majira ya baridi kama silaha ya vita, na kuongeza kuwa ni muhimu kwa Marekani na ulimwengu mzima kusikia moja kwa moja kutoka kwa kiongozi huyo kuhusu vita na umuhimu wa kusimama pamoja kwa mwaka ujao wa 2023.

Comments