RAIS Samia Suluhu Hassan leo atazindua ujazaji maji katika bwawa la kufua umeme kwenye Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) uliopo Rufiji mkoani Pwani, baada ya hatua ya kujenga tuta linalosaidia uhifadhi wa maji katika bwawa hilo kukamilika.
Rais Samia atafanya uzinduzi huo katika hafla itakayofanyika eneo la mradi kwa kubonyeza kitufe kitakachoshusha mageti yatakayoziba njia ya mchepusho wa maji na kuruhusu maji kuanza kujaa katika bwawa.
Hatua hiyo ya kujaza maji katika bwawa hilo lenye ukubwa wa meta za ujazo 32.3, inatazamiwa kutumia misimu miwili ya mvua kukamilisha kujaa na kuruhusu kuwashwa kwa mitambo ya kufua umeme.
Akizungumzia uzinduzi huo, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema hafla hiyo itahudhuriwa na watu wanaokadiriwa kufikia 200 wakiwamo viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na wananchi na ujumbe wa watu 300 kutoka Serikali ya Misri wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ambayo ndiko wanatoka wakandarasi wa mradi huo.
Alisema hatua ya kuzuia mchepusho wa maji ili kuruhusu maji kujaa kwenye bwawa, haitazuia maji ya mto Rufiji kwenda upande wa pili kwa matumizi mengine ya ikolojia na kilimo kutokana na namna mradi ulivyobuniwa.
Alitaja moja ya faida za mradi huo ukiacha kufua umeme ni kwa wakulima wanaolima katika Bonde la Mto Rufiji kwa sababu utazuia mafuriko yaliyokuwa yakisababisha mazao kuharibika na kuanzia sasa maji yatakayoelekea upande wa chini kwa wakulima yatakuwa yamedhibitiwa na kufika kwa kiwango kinachostahili.
Mradi huo unaotarajiwa kufua megawati za umeme 2,115, unatarajiwa kuondoa tatizo la uhaba wa umeme nchini na kupunguza gharama kwa wananchi.
Ongezeko hilo la megawati 2,115 litawezesha Tanzania kujitosheleza kwa mahitaji yake ya umeme na kuwa na ziada ya kuuzwa nje ya nchi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika eneo la mradi, January alisema ujenzi wa bwawa hilo unatekelezwa kwa hatua ambako ili kupata bwawa hilo, ililazimu wakandarasi kuchepusha maji ya Mto Rufiji na kupata eneo kavu la kuchimba handaki na kutengeneza tuta lenye matundu litakaloruhusu maji kujazwa.
Alisema handaki hilo lenye urefu wa meta 700 ndiyo limekamilika na kuruhusu hatua ya kujaza maji kwenye bwawa kuanza na ndiyo itakayozinduliwa leo.
Comments
Post a Comment