Mjue shujaa wa Namibia Hendrik Witbooi

Hendrik Witbooi alizaliwa mwaka 1830, Pella, eneo lililopo mpakani mwa Namibia, ambako kwa sasa ni kaskazini magharibi mwa Afrika Kusini. Witbooi anatokea kwenye mlolongo mrefu wa machifu wa Witbooi Nama, ambalo hapo awali lilikuwa kabila la ufugaji kutoka asili ya watu wa Khoikho wa kusini magharibi mwa Afrika. Mwaka 1863, jamii ya Witbooi Nama ilihamia kwenye eneo ambalo lilijulikana kama Afrika Kusini Magharibi ambalo kwa sasa ni Namibia. Kule, Hendrik Witbooi alipata elimu rasmi kutoka kwa wamisheni wa Kijerumani. Baadaye aliishi kwenye eneo la milimani kusini-magharibi mwa Windhoek, na kuanzisha jamii iliyojipanga vyema ya Nama. Alifariki Oktoba 29, 1905 katika kijiji cha Vaalgras, katika mapigano dhidi ya wakoloni wa Ujerumani.

Hendrik Witbooi alitambulika kwa lipi? 
Alijulikana kutokana na uwezo wa kufikiri haraka, na kutambua mapema jinamizi la ukoloni pamoja na miito yake ya kutaka makabila ya Afrika kuungana pamoja dhidi ya utawala wa ukoloni wa Wajerumani. Ingawa Wanama walikuwa wachache na ambao hawakujipanga vyema ikilinganishwa na majeshi ya Ujerumani, mbinu madhubuti za Witbooi katika kukabiliana na Wajerumani, zilipeleekea kupachikwa jina "the snake in the grass" ama "nyoka kwenye nyasi". 

Aliheshimika na Wajerumani, – mtawala wa kikoloni wa Wajerumani katika eneo la Kusini kaskazini mwa Afrika, Generali Leutwein aliandika kuhusu Witbooi: "bado namuona mbele yangu"…mtu wa kawaida, lakini mwenye kujisimamia, mwaminifu na asiye na hila za kisiasa, kamwe haondoki kutoka kwenye kile anachoamini ni jukumu lake ama haki yake. "Witbooi aliwasiliana kwa kina na viongozi wengine wa Afrika na Ulaya na shirika la kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO imesajili barua zake na shajara (iliyoandikwa kwa lugha ya Kiholanzi) kama miongoni mwa turathi za dunia

Hendrik Witbooi aliweza vipi kuwa alama ya mapambano ya pamoja? 
Wakati Wajerumani walipoendelea kuhodhi maeneo mengi zaidi kusini kaskazini mwa Afrika, Hendrik Witbooi alimuandikia chifu wa eneo jirani wa kabila la Herero. Ingawa kabila la Nama walipigana vita vikali dhidi ya kabila ya Herero, Witbooi alitaka makundi hayo mawili kusimamisha mapigano na kuungana pamoja kupambana dhidi ya ukoloni. Muungano huo kwa kiasi kikubwa ulishindwa – katika kipindi cha muongo mmoja baadaye Wajerumani waliwaangamiza Herero na Nama katika mauaji yaliyotangazwa na Umoja wa Mataifa kama "moja ya mauaji ya mwanzo zaidi ya kimbari katika karne ya 20". Hata hivyo, wito wa Witbooi wa kuungana uliimarisha sifa yake kama kiongozi mkubwa. 

Lakini Hendrik Witbooi hakuwa na mahusiano mazuri na Wajerumani? 
Mnamo 1893, wanajeshi wa Ujerumani walishambulia jamii ya Witbooi, iliyokuwa ikiishi milimani wakiua zaidi wanawake na watoto. Baada ya hayo, Witbooi alisaini mkataba wa ulinzi na Wajerumani. Miaka kumi baadaye, alishirikiana na mamlaka ya kikoloni, hata akiwapa askari wa vita dhidi ya makabila mengine. Alidaiwa kuwa alikuwa na "urafiki mzuri" na Generali Leutwein. Lakini mwaka 1904, Witbooi ilizindua uasi wa kabila ya Nama dhidi ya wakoloni wa Kijerumani, na kuongoza vita vya msituni kwa mwaka mzima kabla ya kujeruhiwa vibaya.

Kauli zipi za Hendrik Witbooi zilizojichukulia umaarufu?
"Hatukuiachia ardhi yetu, na kile ambacho hakikutolewa na mmiliki, haiwezi kuchukuliwa na mtu mwingine."
"Wakati chifu mmoja akiwa chini ya ulinzi wa mwingine, aliye chini hawezi tena kujiongoza, ama kwa watu wake au taifa lake."
Kabla ya kufa kwenye uwanja wa vita, Witbooi alisemekana kuwa aliomba amani: alisema "watoto sasa wanapaswa kupumzika". 

Hendrik Witbooi anakumbukwaje? 
Hendrik Witbooi anasalia kuwa kielelezo cha heshima kwa Namibia katika harakati zake hadi ilipopata uhuru 1990. Sura yake inaipamba fedha ya noti ya Namibia ya $ 50, $ 100 na $ 200 na ari yake ya kimapinduzi na jukumu la kupambana dhidi ya utawala wa Ujerumani pamoja na kutetea nchi yake, bado vinafundishwa na kutambuliwa katika shule za Namibia.

Victoria Averill, Renate Rengura na Gwendolin Hilse walichangia kufanikisha makala haya. Ni sehemu ya makala maalum za mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.

Chanzo: DW Swahili

Comments