TAMASHA la ngoma za utamaduni na maonyesho ya biashara la Mtemi Milambo, linatarajiwa kufanyika Julai 8 hadi 10 kwenye Uwanja wa Chipukizi mjini Tabora. Tamasha hilo lina lengo la kukuza mila na utamaduni kwa makabila ya Tanzania, hususan yale makubwa ya mkoa huo na jirani ya Wanyamwezi na Wasukuma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Chief Promotions, ambao ndio waandaaji wakuu wa tamasha hilo, Amon Mkoga, alisema kuwa tamasha hilo litakuwa ni la aina yake kwa mwaka huu na litasaidia kuenzi na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania, hususan makabila makubwa ya mikoa ya Tabora, Shinyanga na Mwanza, ambako yale makubwa ya Wasukuma na Wanyamwezi yataonyesha bidhaa mbalimbali zenye asili ya Kitanzania, sambamba na michezo ya asili ukiwemo wa bao na kurusha mishale.
Mkoga alisema, shughuli za tamasha hilo zinatarajiwa kuanza asubuhi saa 4:00 hadi 12 jioni kuanzia Julai 8 hadi Jumapili ya Julai 10, ambako wakati wote huo, ngoma mbalimbali zitatumbuiza na kuonyesha utamaduni wake. “Ngoma zitakazotumbuiza ni pamoja na Manyanga, Maswezi, Uyeye, Bagalu, Bagika, Bazuba, Radu na nyingine nyingi, hivyo tunaomba wakazi wa mikoa hiyo kufika kwa wingi ili kujionea, sambamba na kuwaunga mkono katika bidhaa zao,” alisema Mkoga.
Nae, Meneja wa bia ya Balimi miongoni mwa wadhamini wa tamasha hilo, Bi Edith Bebwa alisema kuwa, wamejitokeza kudhaamini kwa mara ya pili mwaka huu ili kuwaenzi wateja wao hao ambao bia hiyo ni mahususi kwa wakazi wa kanda ya Ziwa, “Ngoma hizi za wasukuma na wanyamwezi huchezwa sana wakati wa mavuno, hivyo kwa kuwa Balimi ni bia ya mkulima tumeona tuungane kusherekea pamoja wakati wa mavuno huku tukienzi utamaduni wa Kitanzania” alisema Bebwa.
Aidha, katika tamasha hilo, mgeni rasmi anatarajia kuwa mkuu wa mkoa wa Tabora, Mh Abeid Mwinyimusa, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kushoke kukaya’ yaani turudi nyumbani tafsiri ya Kiswahili toka kinyamwezi. Mbali na kampuni ya bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Balimi, wadhamini wengine ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ubalozi wa Switzerland, Kalunde General Supplies, UNESCO na shirika la ndege la (Fly 540), Geita Goldnes,Magic Fm,Chanel Ten na TBC.
Comments
Post a Comment