HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA, MHESHIMIWA MUSTAFA HAIDI MKULO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2011/2012...!!!
Waziri wa Fedha na Mipango Mh. Mustafa Haidi Mkulo akiwasili Bungeni jioni mjini Dodoma jioni hii tayari kutoa hotuba ya bajeti ya mwaka 2011/2012
Mheshimiwa Spika,
Naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Pamoja na hotuba hii, vipo vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato. Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara na Idara zinazojitegemea ambapo cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2011 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Aidha, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kunichagua kwa mara nyingine tena kuongoza Wizara kubwa na nyeti, ninamuahidi kuwa sitamuangusha. Pia ninampongeza Dkt. Mohammed Gharib Billal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, ninampongeza Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge na kuteuliwa tena na hatimaye kupitishwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi Mhe. Spika Anne Makinda (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Spika na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Bunge katika Afrika Mashariki. Kuchaguliwa kwako kunatokana na imani kubwa waliyonayo Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia busara zako, uwezo na uzoefu wako ndani ya Bunge hili. Napenda pia kumpongeza Mhe. Job Ndugai (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Nawapongeza pia mawaziri wenzangu wote pamoja na Naibu mawaziri wote, kwa kuteuliwa kwao na Mhe. Rais kushika nyadhifa hizo. Aidha, napenda niwapongeze wabunge wote kwa kuchaguliwa na kuteuliwa kuingia katika Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya Bajeti hii. Maandalizi ya Bajeti ya Serikali yanahusisha wadau na vyombo mbalimbali. Kipekee ninaishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda, Mbunge wa Handeni, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya Bajeti hii.
Kwa hotuba kamili
Comments
Post a Comment