Na Mwandishi Wetu
MISS Universe Tanzania 2011, Nelly Kamwelu, amesema ana matumaini ya kufanya vema katika mashindano ya kimataifa ya Miss Universe yanayotarajiwa kufanyika Septemba 12 mjini Sao Paolo, Brazil. Kamwelu alisema, atatumia uzoefu na ujanja alioupata katika Mashindano ya Kimataifa ya Kusini mwa Afrika ‘Miss Southern Africa International’ kama silaha yake katika mashindano hayo.
Kamwelu alisema, amefurahishwa na maandalizi yake na hatokuwa na visingizio endapo matarajio yake yatakwenda kinyume. “Mimi ni miongoni mwa washindani na sitarajii kushindwa, ila endapo kutakuwa na matokeo tofauti, basi itabidi nikubaliane nayo, ila nasisitiza siendi kwa nia ya kushindwa,” alisema Nelly.
Mrembo huyo ambaye aliondoka hivi karibuni, alisema ushindi wa taji la Miss Southern Africa International umemuongezea ari ya ushindi na atajitahidi kwa uwezo wake. Maandalizi ya mrembo huyo ni pamoja na ya kisaikolojia yaliyofanywa na mtaalam Mike Lerch na kampuni yake ya Global MM.Pia mrembo huyo alipewa huduma za kisasa za urembo na mtaalamu gwiji, Patricia Metzger, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya ngozi na kucha.
Pia alipewa ushauri nasaha wa mashindano na mrembo wa mwaka jana Hellen Dausen. Zaidi ya maandalizi ya kimwili na kisaikolojia, Nelly pia amepata msaada mkubwa kutoka kwa wabunifu wa mavazi ikiwa ni pamoja na mbunifu mashuhuri Vida Mahimbo, ambaye amemzawadia ‘kanga jeans’ moja na kaptula moja pamoja na ‘Top 2’ zenye nembo ya Kitanzania na nembo yake ya biashara.
Kamwelu pia alipewa mafunzo ya lugha ya Kireno na wafanyakazi wa ubalozi wa Brazil nchini. Vodacom Tanzania ambao walidhamini pia mashindano ya kumsaka Miss Universe Tanzania, wametoa sh milioni moja, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mrembo huyo, wakati tiketi ya ndege ya Kamwelu imedhaminiwa na Qatar Airways.
Kumpigia kura Nelly bofya hapa.
Comments
Post a Comment