Mh Ngeleja Waziri wa Nishati na Madini akihutubia
Dr Abdelheim Meru kutoka EPZA
Waziri akiwa na maafisa ubalozi na Viongozi wa jumuiya ya Watanzania London
Mh Ngeleja akiwa na mwenyeji wake Balozi Kallaghe(k) na Dr A Meru GD wa EPZA
Waziri Ngeleja akiwa na Mh Naibu Balozi Chabaka wakiteta neno
(Picha na Jestina George & Urban Pulse)
(Picha na Jestina George & Urban Pulse)
**********************
Habari Na Freddy Macha
Wawekezaji, wataalam na wafanyabiashara toka kona mbalimbali ulimwenguni wamekaribishwa kwa mkono wa kheri kuendeleza uchumi na maendeleo ya nchi yetu katika kipindi kinachofuatilia miaka 50 ya Uhuru.
Akiongea wakati wa Kongamano la Uwekezaji (Tanzania Investment Forum 2011) hoteli bab kubwa ya May Fair jijini London jana Ijumaa, Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa William Ngeleja alisema tuko katika kipindi kipya cha maendeleo ya uchumi chenye manufaa kwa wafanyabiashara.
Waziri huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliuambia mkutano kwa Kiingereza fasaha: “Miaka mitatu iliyopita Bongo imebadilika toka mnunuzi wa bidhaa kuwa muuzaji wake. Mathalan siku hizi tunaiuzia Kenya chakula. Ukilinganisha nchi yetu na nyinginezo Afrika , tumekuwa makini shauri ya amani na utulivu miaka 50 iliyopita.”
Hotuba yake mheshimiwa ilikuwa miongoni mwa hoja nyingi zilizochambuliwa na washiriki wazawa wa Uingereza, Norway, Afrika Kusini, Kenya, Marekani, Uholanzi na Tanzania.
Aliwaambia wahusika hapa ughaibuni kwamba taifa letu linafaa sana kuwekezea kwa kuwa tunafuata masharti na maadili ya uchumi wa kimataifa. Kati ya sifa tulizo nazo aliendelea kufafanua, ni kuwepo na demokrasia, serikali bora, kuheshimu sheria (ikiwemo pia sheria za kimataifa za kibiashara), amani na wananchi wanaokaribisha wageni bila ubaguzi.
“Nadhani baadhi yenu mlioshatembelea nchi yetu mmejionea wenyewe namna Watanzania walivyo na hulka nzuri.”
Akijibu swali kuhusu uzorotaji wa njia zinazosaidia shughuli za uchumi mathalan uchimbaji madini, kutokana na ukosefu wa barabara na reli, Waziri Ngeleja alisema mwezi Juni mwaka huu, serikali iliweka Mpango wa Miaka Mitano hadi 2015 unaotazamiwa kukarabati reli zilizopo na kuendeleza pia ujenzi wa barabara na umeme. “Serikali inazingatia sana tatizo la miundo mbinu.”
Mkutano huu wa siku moja ulifadhiliwa na makampuni kadhaa ya kimataifa yakiwemo Aggreko, Trans Allied Resources na Anglo Gold.
Comments
Post a Comment