Jumuiya ya Watanzania London kwa pamoja tunachkua fursa hii kuungana na mamilioni ya watu duniani kote kuwatakia Watanzania wote Heri na mapumziko mema ya sikukuu ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), kwa kutimiza miaka hamsini (50) tangu ilipokabidhiwa uhuru wake tarehe 9/12/1961 kutoka kwa Waingereza.
Jumuiya ya Watanzania London, inawaasa na kuwasihi Watanzania wote duniani kuweza kusherehekea salama na kwa upendo siku ya kesho tarehe 9/12/. Tunawaomba tutunze na tudumishe amani na ushirikiane katika kuijenga nchi yetu kwa hali na mali ili kuweza kufikia malengo ya maendeleo nchini na hata ya millenia kwa dunia nzima.
Jumuiya inapenda kutoa rai kwa viongozi na Watanzania wote ulimwenguni kufanya kila tuwezalo kuhakikisha tunashirikiana katika kuijenga nchi yetu kwa pamoja bila kujali dini, kabila, chama, umri, rangi na jinsia. Tuna amini kuwa kama wote kwa pamoja tutakuwa na nia njema, imani na umoja katika kuijenga nchi yetu kwa kushirikiana basi maendeleo yatapatikana. Kinyume na hivyo miaka itasonga bila kuona mafanikio yoyote.
Tunawaomba Watanzania wote tuishio ughaibuni tuungane na tuwe kitu kimoja kusaidia kupeleka maendeleo nyumbani. Ama tunawaasa tuge mfano kutoka kwa wenzetu kama Nigeria, Ghana, India, Pakistan, Bangladesh na nyinginezo kupeleka maendeleo nchini Tanzania na si kukaa kusubiri viongozi na Watanzania walioko nyumbani kutusaidia.
Tunawaomba Watanzania wote tuwe kitu kimoja, tukijua, kufahamu na kuzingatia kwamba nchi yetu bado inahitaji nguvu za ziada na uwezo wa ziada ili kuweza kufikia malengo ya maendeleo. Pia tunpaswa kufahamu nchi yetu inakabiliwa na matatizo mengi na mitihani mingi katika maisha ya kawaida na hasa maisha ya Mtanzania wa kawaida na ili kuweza kujikwamua yatupasa kujua na kufahamu kwamba hamna mtu mwingine yeyote wa kuweza kubadilisha hali halisi ya maisha yetu bali ni sisi Watanzania wenyewe.
Tunawaomba kwa pamoja tuamke kwa upya na tuweke nguvu kazi zetu kwenye kujijenga na kuijenga nchi yetu kuanzia sasa na kuendelea bila kuchoka wala kukata tamaa, tukijua kwamba maendeleo ya nchi yetu yanatutegemea sisi na sisi tuna jukumu kubwa kwayo.
Kwa mara nyingine tena Jumuiya ya Watanzania London tunawatakia kila la kheri katika siku hii njema ya maadhimisho ya sikukuu ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) na tunawatakia maisha mema wote kwa pamoja popote pale mlipo.
MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATANZANIA WOTE DUNIANI
“HAPPY BIRTHDAY TANZANIA MAINLAND”
Comments
Post a Comment