Wanamuziki wawili wa zamani wa Bendi ya African Stars "Twanga Pepeta" Kalala Junior na Saulo John maarufu kama Ferguson kwa nyakati tofauti walipanda kuimba katika onyesho la Twanga Pepeta lililofanyika jana Jumamosi katika ukumbi wa Mango Garden.
Kwa kuanza alianza kupanda Ferguson kurap nyimbo ya uvumilivu iliyopo katika albamu ya Mtaa wa Kwanza kisha baadae alipanda Kalala kuimba wimbo ambao yeye alishiriki wa Mapenzi hayana kiapo.
Tofauti na Ferguson ambaye alitumia muda mchache sana stejini Kalala alitumia muda mwingi kwa kuanza kuimba kipande chake alichoimba katika wimbo wa Mapenzi hayana Kiapo uliotungwa na Saleh Kupaza, baada ya kuimba akarapu baadhi baadae akaenda sambamba na wanenguaji wa kike kucheza na akamalizia kupiga gitaa la Bass.
Kila mmoja alishangiliwa sana na wapenzi waliohudhuria katika onyesho pale alipopanda na kudhihirisha kukubalika kwao kwa wapenzi wa Twanga Pepeta na kuna baadhi walisikika kumuomba Mkurugenzi wa Bendi Asha Baraka kufikiria kuwarejesha kwenye Bendi ili pamoja na waliopo wazidi kuiimarisha Twanga Pepeta.
Wanamuziki hao waliihama Twanga Pepeta katika kipindi tofauti mwaka jana na mwaka juzi ambapo alianza Kalala kuondoka mwaka juzi kwenda kuanzisha Bendi ya Mapacha watatu akiwa na wenzake Jose Mara na Khalid Chokoraa baadaye aliondoka Ferguson kwenda Extra Bongo.
Comments
Post a Comment