SIWEZI KUKULILIA KWANI HAKUNA NINACHODAI TOKA KWAKO, TANGULIA TU STEVEN KANUMBA by RAMA S. MSANGI...!!!
Mbeya – Tanzania,
09/04/2012
Ni asubuhi na mapema sana, jumamosi ambayo nilichelewa sana kuamka kwani haikuwa siku ya kazi na pia nilikawia sana kulala. Na miongoni mwa sababu zilizonifanya nichelewe kulala, ilikuwa ni filamu ya “Kijiji Tambua Haki”, ambayo jioni ya Ijumaa, tulipitia mahali mimi na mwenzangu, tukainunua.
Naam, asubuhi hii ninapikurupuka usingizini, nakuta ka BB kangu kanawaka taa nyekundu mfululizo tu, najiuliza kuna mtu kanipigia sikuisikia au ni ujumbe mfupi au ni nini hasa? Naam, ninanyoosha mkono na kuiokota, na ninapoicheki, nakutana na ‘notifications’ za kumwaga, na ninaamua kuanza kwanza kusoma barua pepe kabla ya sms na mengineyo.
Ninapofungua tu box labarua hizo, nakutana na vichwa vya barua hizo kama 10 vyote vikiwa na neno Kanumba. Nafikicha macho kwa uzuri na kuamka kukaa kitandani kwanza, kisha naanza kupekua. Naam, ndipo hapa ninakumbana na habari za kushtusha sana. Steven Charles Kanumba, amefariki dunia.
Kwanza nilikimbilia kalenda yangu, kuangalia ilikuwa tarehe ngapi, nilijua ni April mosi, na nilisahau ghafla kuwa tulikuwa kwenye wikiendi ya sikukuu ya Pasaka. Na ninapobaini kuwa sio siku ya wajinga, narejea kwenye simu yangu na kusoma kila kitu. Na kila kitu nilichokisoma kilihusiana na kufariki kwa msanii nguli wa filamu nchini Tanzania, Steven Kanumba.
Baada ya hapo, niliwapa taarifa wanafamilia wenzangu, ambao kila mmoja alishikwa na butwaa kwa dakika kadhaa huku kila mmoja akidhani natania. Ndio, walikuwa na sababu ya kudhania hivyo. Maana ni jana yake sote tulikawia kulala tukitizama filamu, ambayo sasa naweza kuiita ya mwisho iliyokuwa iko sokoni ya msanii huyo. Kijiji Tambua Haki.
Ninapiga simu kwa watu wangu kadhaa ambao ninaamini kama vyanzo vyangu vya uhakika na ninathibitishiwa kuwa kweli Kanumba hatunaye. Ninashusha pumzi, ninazivuta na kuzishusha tena, kisha ninakimbilia bafuni kuswaki, kuoga na kuhamishia maskani sebuleni kwenye luninga kuangalia yaliyokuwa yakijiri kuhusiana na suala hilo. Na ndipo hapo hali ya kuamini inazidi kuniingia.
Hali Halisi:
Ilivyo ni kwamba, kupitia kazi zake, hakika sidhani kama kuna ambalo sijalijua kuhusu uwezo wake, lakini siwezi kuwa mnafiki na kutamka hapa kwamba nilikuwa namfahamu sana, kwahiyo jambo la kwanza nililolifanya ilikuwa kuanza kupekua pekua kwenye vyanzo mbalimbali ili kupata historia yake japo kwa kifupi sana.

Ni kupitia kwenye pekua pekua hiyo ambapo nilibaini kuwa filamu ya ukweli ya maisha ya Steven Kanumba ilianza rasmi Agosti 12, 1984, mkoani Shinyanga, pale alipowasili hapa duniani kupitia kwa tumbo la bi. Flora Mtegoa. Baada ya hapo akapata elimu yake kupitia shule mbalimbali kuanzia huko huko Shinyanga hadi jijini Dar es salaam, ambako pia maisha yake ya usanii yalianza, kushamiri na hatimaye kuzimika ghafla hivi karibuni.
Huyu ni kijana ambaye usanii aliuanza mapema sana akiwa bado mdogo, kwa kujiunga na vikundi vya uigizaji kupitia luninga kabla ya baadae kuachana na uigizaji wa maigizo ya luningani ya kila wiki na kuzama kwenye kucheza filamu. Na ni huku ambako aliweza kuuteka umma wa Watanzania kupitia kazi zake mbalimbali zilizokuwa katika ubora wa aina yake.
Katika filamu takriban 40 na ushee ambazo aliweza kuzifanya enzi za uhai wake, sote tunajua ni kwa namna gani Kanumba alikuwa akikumbana na vikwazo vya aina mbalimbali. Wapo waliomponda kuwa alikuwa akiiga kazi fulani fulani, wapo waliokuwa wakimponda kwa kila hali, lakini mwisho wa siku ni Kanumba huyo huyo ambaye alifanikiwa kupasua anga kimataifa zaidi na kufanya filamu na wasanii wenye kuheshimika barani Afrika na hata duniani kwa ujumla.
Dunia yamlilia:
Naam, taarifa za kufariki kwa Kanumba, zilisambaa ghafla dunia nzima. Nikapokea simu, barua pepe na mawasiliano mengine toka sehemu mbalimbali za dunia, nikiulizwa juu ya hilo. Naam, ghafla nilipoanza kufuatilia yanayojiri kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, ndipo nagundua ni kiasi gani dunia inamlilia Kanumba. Huyu alishakuwa zaidi ya Mtanzania. Alishakuwa msanii wa kimataifa zaidi na kazi zake zilisambaa karibu kila pembe ya dunia hii, na kwakuwa zilikuwa na ubora, haishangazi watu kumlilia.

Kwanini siwezi kumlilia:
Kutoka mtoto wa kawaida hadi shujaa anayeliliwa na taifa zima na hata nje ya mipaka ya nchi yetu, Steven Kanumba, ni mwendelezo wa maandiko ya dini mbalimbali kwamba mwanadamu ameletwa duniani na muumba wake kwa malengo maalum. Kupitia kwake tunajifunza kuwa, kila tunayemuona kuwa na mafanikio sana, ni binadamu kama walivyo binadamu wengine na ambaye mwanzo wa maisha yake huwa ni wa kawaida kama walivyo wanadamu wengine.

Kupitia kwa Kanumba, tunajifunza kuwa, kumbe kila mwanadamu ana uwezo wa kuifanya dunia imtambue na kumthamini kwa mafanikio yake bila hata kujali alitokea katika mazingira ya shida au laa.
Kanumba alikuwa mmoja wa walioifanya tasnia ya filamu nchini kufikia hapa ilipo, na kupitia kwake tunajifunza kuwa kumbe kila mwanadamu duniani akiamua kuachana na maneno yanayotaka tu kumkwaza ndoto zake, kama ambavyo yeye alikuwa akikumbana nayo, basi anaweza kulifanya jangwa kuwa nchi ya kijani iliyojaa neema za kila aina. Kupitia kwa Kanumba, tumeweza kujua kuwa kumbe hata uuzaji sura nao ni ajira tena ajira ya maana sana. Naam, kupitia kwa Kanumba, tumejifunza mengi ambayo ni vigumu kuyaeleza hapa yote kwa wakati huu.
Kama ambavyo maandiko hutuaminisha, kila mwanadamu huletwa duniani kwa sababu na kazi maalum. Ninaamini kabisa kuwa Kanumba ametimiza malengo aliyokuwa amewekewa na muumba wake katika ulimwengu huu. Kuelimisha, kufundisha, kuburudisha, kuwa kioo cha kujitizamia lakini zaidi ya yote, kuwa mfano mwingine wa namna gani maisha ya mwanadamu yanatakiwa kuwa ya kujiandaa kwa safari ya kurejea kwa muumba wetu siku na wakati wowote ule.
Naam, kama ni lipi ambalo nitakuwa namdai kijana mwenzangu huyu Steven Kanumba? Amenifundisha uwepo wa Muumba kupitia ujio wake duniani, amenikumbusha uwepo wa Mungu na nguvu zake kupitia kifo chake, ameniburudisha kupitia kazi zake, amenifundisha kupitia kazi zake, amenifanya nione jinsi gani mtu mmoja anaweza kuibadili jamii kama akidhamiria. Kipi kingine kilichobakia? Ninaamini hakuna katika yale ambayo alielekezwa na Mungu kuja kunifundisha, ambalo ameliacha. Sasa ni kipi ninachomdai hapo?
Hakika hakuna ninachomdai Steven Kanumba, hakika sina sababu ya kumlilia, bali nitanyoosha mikono yangu miwili juu na kusema “Asante Mwenyezi Mungu kwa kila ulilolitenda kwa Kanumba. Nashukuru ulimleta ulimwenguni katika Tanzania yetu, nashukuru kuwa ulimuelekeza atuelimishe kwa kazi zake na kwa njia ambayo sote tulimuelewa, na nashukuru kuwa umemchukua baada ya ulichomtuma kukamilika. Wewe ni mkuu kuliko wote na kazi yako haina makosa. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu, tunakuomba umpe mapumziko yenye amani milele mja wako Steven Charles Kanumba”
Rama S. Msangi,
Founder, Admin & CEO,
Jukwaa Huru Media,
Comments
Post a Comment