HAKI ZA WANAWAKE KATIKA KATIBA YA NCHI...!!!

Women Fund Tanzania (WFT)
Empowering Local Woman Heroes
Kuwezesha Wanawake Shujaa

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Haki za Wanawake katika Katiba ya Nchi

Dar-es-salaam (Tanzania), Oktoba 15, 2012 – Tangu 2011, Tanzania imekuwa ikiendesha mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba ya nchi katika jitihada za kutengeneza katiba mpya ifikapo 2015. Asasi ya Women Fund Tanzania (WFT) (au Mfuko wa Wanawake Tanzania), iliyojikita katika kutetea haki za wanawake nchini, ikishirikiana na wadau wengine walio katika harakati hizi, wameandaa mkutano wa siku tatu utakaojadili maswala muhimu ya wanawake katika katiba mpya. Mkutano huo utafanyika Oktoba 22 hadi 24, 2012, katika hoteli ya Blue Pearl Ubungo, Dar es Salaam.

Washiriki wa mkutano huo wanatoka katika nyanja na mashirika mbali mbali nchini na wataibua na kujadili mapungufu yaliomo katika katiba ya sasa, na kutengeneza mikakati ya kuyashughulikia mapungufu haya. Wanaharakati wanawake na wakereketwa wa maswala ya haki za wanawake wanatarajiwa kwa pamoja kuainisha maswala muhimu ya wanawake yanayostahili utetezi ili yazingatiwe katika katiba mpya.

Mkurugenzi wa WFT, Mary Rusimbi amesema: “Mkutano huu unatoa nafasi muhimu kwa wanawake kujadili kwa kina na kuimarisha uelewa wao juu ya maswala nyeti yanayogusa haki zao katika mchakato unaoendelea hivi sasa. Pia ni fursa kwa wanawake kujifunza mbinu zinazokubalika katika kujenga sauti moja na msimamo wa pamoja katika mchakato huu.”

Asasi ya WFT na washirika wake wanaendeleza harakati hizi kutokana na umuhimu wa ushikishwaji wa wanawake katika maswala ya kikatiba na hasa katika nchi ambayo bado ina baadhi ya sheria i zinazomkandamiza mwanamke.

Katiba ya sasa ya Tanzania ya mwaka 1977 inadai kutomkandamiza mwanamke kwa jinsi yake au jinsia, japokuwa kuna sheria kadhaa zinazotoa kipaumblele kwa taratibu za kimila, na hivyo kutozingatia haki za wanawake. Sheria hizi zinahusu maeneo mbalimbali kama vile ndoa, talaka, afya ya uzazi, elimu uongozi, siasa, na maswala ya kujikimu kimaisha.

Wanawake 100 kutoka Tanzania bara na Zanzibar, wamealikwa kuhudhuria mkutano huo unaotarajiwa kutoa mpango kazi utakaoongoza harakati za kutetea haki za wanawake katika katiba mpya.

Washiriki watatokea makundi mbalimbali yakiwemo yale ya kijamii, ya kibiashara, vyama vya wafanyakazi, taasisi za elimu ya juu, vyama vya kisiasa, mashirika ya kidini, vyombo vya habari, teknologia ya habari, asasi za mazingira, afya, utamaduni, na wafanyabiashara.

Kuhusu Asasi ya Women Fund Tanzania (WFT)
WFT inatoa nafasi na utaratibu wa kusaidia makundi yasiyosikika na yasiyo na uwezo ikiwa ni pamoja na kutoa fursa ya kuyapa kipaumbele maswala yanayohusu wanawake. WFT ina utaratibu unaorahisisha kusaidia makundi haya ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo katika ngazi mbali mbali. Kwahiyo, WFT imeanza kuchangia na kuimarisha harakati za wanawake nchini na nje ya nchi. Asasi hii illisajiliwa nchini mwaka 2008 chini ya Sheria ya Makampuni ya 2002, kama asasi ya kijamii itakayoshughulikia maswala ya haki za wanawake. Asasi inayoshirikiana na WFT ilisajiliwa nchini Uholanzi kama kwa madhumuni ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji was shughuli za WFT. Asasi ya WFT imeanzishwa wakati ambapo harakati ya kutetea haki za wanawake zimeanza kupata nguvu mpya. Kwa mantiki hiyo, inajumuisha nguvu za harakati hizi, kuimarisha, na kuwa sehemu ya msukumo huu wa kuhakikisha kwamba haki za wanawake zinazingatiwa katika maswala yote. Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2007/2008, WFT imekuwa ikijishirikisha katika kutafuta na kukusanya michango ya mawazo kutoka kwa wadau wanaojihusisha na maswala ya haki za wanwake ndani na nje ya nchi, na yote haya yamekuwa muhimu katika kutathmini uwezekano wa kuendesha asasi hii nchini, kuifanya iwe endelevu na kuongoza utekelezaji wa mipango yake.   Kwa maelezo zaidi tembelea: : http://womenfundtanzania.org

PICHA NA MENGINEYO DOKOA HUMO

Comments