WAZIRI MWAKYEMBE ACHANGAMKIWA NA JUMUIYA YA WAINGEREZA NA WATANZANIA LONDON...!!!

Waziri wa Uchukuzi Tanzania, Mheshimiwa Dr. Harrison G. Mwakyembe- (Mbunge), akihutubia kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Waingereza waliowahi kuishi nchini Tanzania (Britain Tanzania Society(BTS)). Mheshimiwa Waziri Mwakyembe alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano huo wa Mwaka wa Taasisi hiyo ya BTS yenye kutoa misaada mingi kwa Tanzania, kama vile Vifaa vya kusomea, Ujenzi wa Shule, Vifaa vya Mahospitalini, uchimbaji wa Visima na kusaidia upatikanaji wa maji safi,misaada ya Kitaalam kwa Tanzania kwa ujumla.
 Sister Lucia akiuliza swali kuhusu ajali ya meli Zanzibar
Watanzania na baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya BTS, wakizikiliza kwa Makini Hotuba iliyokuwa ikitolewa na mgeni rasmi Mheshimiwa Waziri Dr. Harrison Mwakyembe kwenye Mkutano mkuu wa Mwaka, siku ya jumamosi 10 Novemba 2012
 Mwakyembe akisikiliza hoja baada ya kikao

 Aseri Katanga akiwa mjadalani kwa chai na Billy Mwangamilo na George Kantande
 Yusufu Kashangwa akijadiliana na Waziri huku kasikilizwa kwa uchu na wananchi wengine
 Mtayarishaji wa mkutano Andrew Coulson akipiga gumzo kwa chai na mmoja wa wahudhuriaji
 David Luhanga na Rajab Juma wamekita ndani ya maongezi
 Dk Hamza na wenzake katika chai
 Waziri na wananchi wa kila rangi na jinsia katikati ya maongezi
 Mjadala uliomzunguka Waziri
Rashid Dilunga akiwa kazini
Mheshimiwa Waziri Mwakyembe, Mheshimiwa Balozi wa Tanzania, London (Mhe. Peter Kallaghe), wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Watanzania waliohudhuria kwenye mkutano wa Jumuiya ya BTS, siku ya jumamosi, terehe 10 Nov 2012, kwenye Ukumbi wa Westminster City Hall, London
---

Habari na Picha kwa hisani ya Freddy Macha na Rashid Dilunga

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewahakikishia Watanzania na wageni  kwamba jitihada zitaendelea kufanywa na serikali kuboresha usafiri Bongo.
Akiongea mjini London juzi katika “mkutano wa mwaka” wa jumuiya ya Watanzania na Waingereza (Britain-Tanzania Society) na Mfuko wa Udhamini wa Maendeleo  (Tanzania Development Trust), alisema bado pana mengi sana ya kufanya toka ateuliwe miezi minne iliyopita.
Waziri Mwakyembe vile vile alifafanua kuhusu  majadiliano ya katiba mpya inayotegemewa  kutajwa mwaka 2015.
Akijibu maswali toka kwa Wazungu na Watanzania waliohudhuria kikao   Central Hall, Westminster, hatua chache karibu na Ikulu ya Uingereza (Whitehall), Mwakyembe ambaye ni mbunge wa Kyela, alifahamisha kuwa moja ya tatizo lililojaribu kutafutiwa ufumbuzi karibuni ni kuzorota kwa bandari ya Dar es Salaam. Alisema Wizara ilibidi kubadili uongozi wa bandari hiyo baada ya ripoti ya kimataifa iliyoichamba Dar kuwa moja ya bandari mbaya duniani zisizotekeleza kazi zake sawasawa.
“Bandari ya Dar es Salaam  ina uwezo wa kulisha uchumi wa nchi nzima ikiendeshwa vyema,” aliueleza mkutano uliomsikiliza kwa makini. “Tumezungukwa na nchi nyingi zisizo na bahari ambazo zinatutegemea kusafirisha mizigo yake. Kwa hiyo basi, wizara ya uchukuzi ikilala na taifa zima linalala.”
Akitoa mifano kadhaa ya hali mbaya ya usafiri nchini,  Dk Mwakyembe aliongelea kwa hamasa na matumaini kuhusu ujenzi wa barabara na  reli mbalimbali. “Tuna mengi bado ya kufanya. Reli zetu kubwa ni za kale sana. Ya toka Dar hadi Kigoma na Mwanza mathalan ilijengwa enzi za Wajerumani kwa hiyo yabidi kutengenezwa upya.”
Alitoa mfano wa ufumbuzi wa tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam ambapo pesa zilizopangwa kurekebisha njia nyingine mikoani zimetumika kurahisisha  usafiri kati ya Ubungo hadi mjini na Makanga hadi Kurasini ( kwa nauli nafuu ya shilingi 500) na muda mfupi wa dakika ishirini.
Akiwaelemisha waliokuwepo kuhusu maendeleo ya kisiasa Tanzania, Waziri alisema mjadala unaosisimka nchini sasa hivi unahusu mageuzi ya katiba ambayo “inatakiwa ioane na maisha ya karne ya 21.”
Akifafanua  historia ya katiba Tanzania kwa lugha ya fasaha ya Kiingereza, Waziri huyu ambaye  ni mtaalamu wa sheria, alitaja miaka muhimu kuwa 1961( baada ya Uhuru),1963 (Ujenzi wa taifa jipya), 1965 (Muungano),  1977 ( kuzaliwa CCM) kisha 1983 na  kupitishwa sera ya vyama vingi mwaka 1992.
Maswali mengi yaliulizwa kuhusu usafiri na ulaji rushwa uliochangia sana uzorotaji unaoendelea kusababisha ajali kubwa na za kutisha bara na visiwani.
Na hata baaada ya hotuba rasmi, wakati wa kupata chai, wananchi na wageni  waliendelea kumsonga na kumzunguka Waziri wakimjuza kwa maswali  moto moto. Kiongozi  hakuonyesha dalili zozote za kuchoshwa na shauku hiyo.
Akimshukuru Waziri, mmoja wa maofisa wa Jumuiya ya Waingereza na Watanzania, Bi. Valerie Leach (anayeendesha shughuli za kielimu Bongo) alisema inawapa wageni moyo kwamba Tanzania inao viongozi wanaokinzana na rushwa na ufisadi kama ilivyokuwa enzi zile za Mwalimu Nyerere.
Mapema Dk Harrison Mwakyembe  alikaribishwa kwa maelezo ya namna alivyoshaokoka kufa mara mbili (ajali ya gari na maradhi ya ngozi) kutokana na msimamo wake kujaribu kuendeleza jamii.
Mapema  mkutano ulielezwa miradi mbalimbali inayoendelezwa na Mfuko wa Udhamini wa Maendeleo  (Tanzania Development Trust). Kati ya miradi hiyo ni kukarabatiwa nyumba ya wazee Tanga, uendelezaji wa viwanda vidogo vidogo 37 bara na visiwani,  maendeleo ya vijana wasiokuwa na kazi na vifaa vya wafanyakazi wa hospitali ya Lindi kuepuka kipindupindu.
Akielezea mapenzi yake kusaidia maendeleo Tanzania, mwanamakati wa Jumuiya ya BTS, Julian Marcus alisema jitihada za wanachama zinatokana na michango binafsi na kujitolea bila malipo yeyote.
Shughuli hii ya Jumamosi vile vile ilihudhuhuriwa na Balozi wetu Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe na Mkurugenzi wa kituo cha biashara London, Yusufu Kashangwa.
Jumuiya ya BTS ilianzishwa mwaka 1975 na Waingereza na Watanzania kuendeleza mahusiano kati ya nchi hizi mbili. Inaongozwa na Rais wa zamani, Ali Hassan Mwinyi.
Kikao kijacho cha BTS kitafanyika chuo kikuu cha lugha za Kiafrika na Asia (School of Oriental and African Studies-SOAS) London kujadili demokrasia na vyombo vya habari Tanzania, tarehe 6 Desemba. Kila mwananchi na rafiki wa Tanzania anakaribishwa.

Habari zaidi www.btsociety.org
Au wasiliana na Andrew Coulson – simu (+44) 121-475-4615
Barua pepe: a.c.coulson@bham.ac.uk


Tovuti: www.freddymacha.com

Comments