MHE. ZITTO KABWE AZUNGUMZIA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE...!!!

Matokeo ya Kidato cha Nne ya namna hii (zaidi ya nusu ya wahitimu kupata sifuri) na takribani asilimia 90 kufeli kwa kupata daraja la nne na daraja la sifuri ni mwaka tatu sasa mfululizo. Matokeo yakitoka tunasema weeee mpaka povu linatoka. Baada ya wiki tumeshasahau na hakuna hatua yeyote. Lazima Uwajibikaji utokee.

Kwanza Waziri lazima awajibike na Naibu wake na Katibu Mkuu na Kamishna. Najua kuwa haina uhusiano wa moja kwa moja maana matatizo ya elimu ni makubwa sana nchini. Lakini ni lazima kitu fulani kitokee ili kufanya mabadiliko. Uwajibikaji ni njia mojawapo inayoleta nidhamu na 'urgency' katika utendaji kazi.

Tumwambie Rais aichukue Wizara ya Elimu, yaani Waziri wa Elimu awe yeye (kuwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Elimu). Tumwambie matokeo yakibaki hivi mwakani na yeye atatoka. Najua wa mwakani ndio wapo kidato cha nne sasa na wana msingi mbaya tayari lakini sio jukumu letu kujipa majibu bali ni jukumu letu kuiambia Serikali hapana. Tuwape Masharti. Vinginevyo haya yatakwisha na mwakani itakuja nk.

Hawa watoto wanakwenda wapi? Mwaka jana tulisema mpango wa kujenga vyuo vya ufundi kila Halmashauri ya Wilaya uanze mara moja. Katika Bajeti Kivuli mwaka 2011 tulipiga hesabu kwamba tunahitaji tshs 720 bilioni katika kipindi cha miaka 5 ijayo kujenga vyuo vya ufundi vya VETA kila Wilaya. Tukawaambia badala ya kukopa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kulipana posho ni vema tukope kuwekeza kwenye elimu maana Elimu ni Hifadhi ya Jamii. Elimu yetu ya sasa inazalisha matabaka kwneye jamii na ni hatari sana kwa uhai wa Taifa.

Tunaweza kujidai kujenga madaraja na miji mipya. Tunaweza kujidai kujenga mabomba ya gesi na kusambaza umeme kila kijiji mpaka kwenye vyoo. Kama hakuna Elimu haya yote ni bure kabisa. Hata kukosa uvumilivu wa kiimani sasa hali itakuwa mbaya zaidi unapokuwa na Taifa la mambumbumbu. Waziri Kawambwa na wenzake watoke. Watoke SASA.

Kumekuwa na maoni mengi sana kutoka kwa wadau mbali mbali pia kuhusiana na matokeo hayo ambayo yanasikitisha sana na hapa chini ni maoni ya Dr. Ida ambayo nakubaliana nae 100% ya kwamba ni lazima mfumo wa Elimu Tanzania uangaliwe na kupangwa upya. 
Je wewe mdau wa blogu hii una maoni gani juu ya mfumo wa elimu Tanzania na matokeo haya yasiyo ridisha? "Sema usikike" kwa kuacha maoni yako.


Tazama matokeo ya  NECTA 2012 O Level kwa ku BOFYA HAPA (shukurani kwa JamiiForums.com)



Comments