Dar es Salaam 8th February 2013….Fedha taslimu shilingi milioni 5 zimekabidhiwa kwa lengo la kuwezesha ufanikishaji wa mafunzo kwa Wakunga waliopo hospitali ya Kisarawe mkoani Pwani yatakayojikita katika kukabiliana na vifo vya akinamama na watoto wakati wa kujifungua.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza kutolewa wakati wowote kuanzia sasa chini ya uwezeshaji wa Chama cha Uzazi na Malezi Bora nchini (umati) ambayo yatashirikisha wakunga na baadhi ya wauguzi kutoka ndani ya hospitali hiyo kwa awamu ya kwanza ya majaribio na baadaye kusambaa maeneo mengine ya mkoa huo
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya hundi hiyo kwenye hospitali ya wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani jana, Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatma Kimario, alisema msaada huo umekuja wakati muafaka wakati serikali iko katika harakati za utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kuboresha afya ya mama na mtoto sanjari na kuhakikisha inapunguza vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kadiri inavyowezekana
“Tunawapongeza sana Vodacom kwa uwezeshaji huu unaoambatana na kuunga mkono harakati zilizopo za serikali za kukabiliana na changamoto za afya ya mama na mtoto, tunaomba kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo mtutazame pia kwenye maeneo mengine yakiwemo ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na upatikanaji wa vifaa tiba na maabara ya kisasa,” alisema Kimario
Naye Mganga Mkuu wa Hospital ya Wilaya hiyo, Dr, Msengi Mwendo alisema msaada huo unatarajia kuongeza ufanisi kimafunzo sanjari na kuboresha huduma za afya kwa hospitali hiyo ambayo hutoa huduma za kujifungua kwa akinamama wapatao takribani 350 kwa mwezi.
“Tunaamini msaada huu utatusaidia kwa kiasi kikubwa katika ustawishaji wa taaluma kwa wakunga katika Nyanja za kupeana na kubadilishana ujuzi na maarifa kwa lengo la kupunguza na ikiwezekana kutokomeza changamoto zinazoikabili afya ya mama na mtoto hususan wakati wa kujifungua.” alisema Mwendo
Aliongeza kuwa kwa sasa bado hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo uhaba wa ofisi na vifaa tiba jambo linalopelekea madaktari wapatao 16 waliopo hospitalini hapo kuhudumia wagonjwa wengi huku wakiwa kwenye vibaraza na katika mazingira magumu na wakati mwingine kulazimika kuwahamishia hospitali nyingine
Aliongeza kwa kuwaomba Vodacom na wadau wengine kushirikiana nao katika uboreshaji wa miundombinu ya hospitali hiyo iliyojengwa takribani miaka 50 iliyopita kwani kwa sasa inahudumia wakazi zaidi ya laki moja kutoka ndani na nje ya Kisarawe huku ikiwa na ofisi moja ya daktari na wodi chache zisizotosheleza mahitaji ya wagonjwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Jamii wa Vodacom, Yessaya Mwakifulefule, alisema wanatambua umuhimu na thamani ya afya ya mama na mtoto ndani ya jamii ndio sababu wamesukumwa kuchangia.
Alisema kwa kutambua tatizo hilo Vodacom wameamua kuungana na ‘Umati’ kwa kutoa msaada huo ili kukabiliana na changamoto iliyopo, kwa kuzingatia nafasi na umuhimu wa mwanamke ndani ya jamii na stahiki zake ikiwemo upatikanaji wa huduma bora ya afya na hasa ile inayotolewa na wakunga.
Wakati mwingine hatua ya akinamama kujifungulia nyumbani haitokani na imani potofu au elimu duni bali hutokana na umasikini uliokithiri na wakati mwingine umbali mrefu kutoka nyumbani hadi kilipo kituo cha afya sambamba na usafiri usioaminika au ubovu wa barabara.
Mwakifulefule alisema pamoja na mambo mengine azma yao ni kuhakikisha wanaifikia jamii katika maeneo yote, kuijali, kuisikiliza na kusaidiana katika kutatua kero na changamoto zinazoizunguka.
Alisema changamoto ya vifo vya akinamama na watoto ni ya jamii nzima, hivyo msaada uliotolewa anaamini kwa kiasi kikubwa utasaidia kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akisisitiza kuwa kama mkunga akiwezeshwa ni dhahiri afya na uhai wa jamii nzima utakuwa salama.
“Kwa kutambua umuhimu wa afya ya mama na mtoto na changamoto za kukabiliana nayo tumeamua kukabidhi kiasi hiki kwa majaribio ya mpango huu na baadaye maeneo mengine kwa Kisarawe yote, tunaahidi kuendelea kuwa karibu katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili afya ya mama na mtoto,” alisema Mwakifulefule
----
Meneja Biashara idara ya uhusiano wa Vodacom Tanzania, Lillian Kisamba(kushoto), akishiriki kumkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 5 Mkuu wa wilaya yaKisarawe Bi FatmaKimario (kulia). Fedha hizo zimetolewa na Vodacom Foundation wilaya ni hapo jana kwa ajili ya kuwezesha ufanikishaji wamafunzokwaWakunga waliopo hospitali ya Kisarawe mkoani Pwani.Katikati niMkuu wa kitengo cha Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule, na wengine wanaoshuhudia ni wakunga na maofisa uuguzi wa hospitali hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation Yessaya Mwakifulefule (katikati) akimpongeza Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Bi FatmaKimario (kulia) muda mfupi baada ya kumkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 5 wilayani hapojana, kwa ajili ya kuwezesha ufanikishaji wa mafunzo kwa Wakunga waliopo hospitali ya Kisarawe mkoani Pwani,kushoto anayeshuhudia ni Meneja biashara Idara ya uhusiano wa Vodacom Tanzania, Lillian Kisamba.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bi Fatma Kimario (kulia) na Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kisarawe, Dk Msengi Mwendo (kushoto), wakitazama mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 5 waliyokabidhiwa na Vodacom Foundation wilayani Kisarawe jana, kwa ajili ya kuwezesha ufanikishaji wa mafunzo kwa Wakunga waliopo hospitalini hapo, katikati pamoja nao ni Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation, Yessaya Mwakifulefule
Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Bi Fatma Kimario (kulia), akimsikiliza afisa utetezi wa chama cha uzazi na malezi bora nchini (umati), Bi Easter Mwanjesa (kushoto), kwenye hospitali ya wilaya ya Kisarawe muda mfupi baada ya Vodacom Foundation kukabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 5 jana, kwa ajili ya kuwezesha ufanikishaji wa mafunzo kwa Wakunga waliopo hospitalini hapo, mafunzo hayo yatatolewa na umati.
Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation Yessaya Mwakifulefule (kulia) akizungumza na maafisa wauguzi waandamizi na wakunga wa hospitali ya wilaya ya Kisarawe muda mfupi kabla ya kukabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuwezesha ufanikishaji wa mafunzo kwa Wakunga waliopo hospitali ya Kisarawe mkoani Pwani, wa pili kutoka kulia ni Meneja wa biashara ndani ya idara ya uhusiano wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom, Lillian Kisamba.
Afisa uuguzi wa hospitali ya wilaya ya Kisarawe, Bi Anicia Alute (kushoto), akiwaeleza baadhi ya maofisa wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom waliofika hospitalini hapo changamoto mbalimbali na mikakati waliyonayo katika kukabiliana na vifo vinavyohusisha afya ya mama na mtoto, katika tukio hilo Vodacom Foundation ilikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh milioni 5 ili kufanikisha mafunzo yanayotarajiwa kutolewa kwa wakunga wa hospitali hiyo kwa malengo ya kukabiliana na changamoto za afya na uzazi. Kutoka kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation, Yessaya Mwakifulefule na Meneja wa Biashara wa idara ya uhusiano wa Vodacom, Lillian Kisamba
Comments
Post a Comment