Jahazi iliyokuwa ikitokea Pangani mkoani Tanga kwenda Zanzibar ikiwa na watu 32 juzi usiku ilizama katika eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Zanzibar ambapo watu 10 wanahofiwa kuwa wamepoteza maisha.
Taaarifa tulizozipata zilisema kati ya abiria 27 na wafanyakazi watano waliokuwa kwenye boti hiyo, ni watu 20 tu waliokuwa wameokolewa wakati wengine 10 wakiwa hawajulikani walipo.
Msemaji wa Mkuu wa Polisi nchini, Advera Senso alisema jahazi liitwalo Sunrise liliondoka Tanga juzi saa 2:00 usiku kuelekea Zanzibar, lakini lilipigwa na dhoruba katika eneo la Nungwi.
“Mpaka sasa watu 22 wameokolewa akiwamo nahodha Abdallah Selemani, kumi wanatafutwa ijapokuwa wanahofiwa kuwa wameishakufa. Kati ya hao ni watoto watatu na watu wazima ni saba,”alisema Senso katika ujumbe alioutuma kupitia simu yake ya mkononi.
Nahodha wa Jahazi ya Sun Rise, iliyozama kati ya Tanga na Mkokotoni, karibu na Mkondo a Nungwi, Abdulla Saleh, akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, jinsi mkasa huo ulivyowatokea na kuzama baada ya chombo chao kupatwa na dhoruba kali.
Hata hivyo idadi ya watu waliookolewa kwa mujibu wa Senso ilitofautiana na ile iliyokuwa imetolewa awali na Kamanda wa Wanamaji na Bandarini Zanzibar, SP Martin Lisu aliyesema juhudi za kuwaokoa abiria hao zilikuwa zikiendelea na kwamba waliokuwa wamepatikana wakiwa hai ni watu 21.
Lisu alisema abiria hao walionusurika kifo walipelekwa hospitalini kwa ajili ya kuchunguzwa afya zao na wengine walipatiwa huduma za kwanza kutokana na mshtuko walioupata.
Kusema kweli tulifanikuwa kuwaokoa abiria 21 na wengine siwezi kusema kama wamezama ila nachoweza kusema ni kwamba bado hatujawapata,” alisema Kamanda Lisu na kuongeza:“Taarifa nilizonazo ni kwamba, hii boti ilikuwa ikitokea Pangani, ilipofika eneo la Nungwi ikakubwa na dhoruba kali na kisha kuanza kupoteza mwelekeo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akimfariji mmoja kati ya abiria waliokua katika Jahazi la Sun Rise, Juma Ali Jaku , iliyopata ajali na kuzama kati ya Tanga na Mkokotoni karibu na Mkondo wa Nungwi, ikiwa imebeba jumla ya abiria 32 kati ya hao 21 wameokolewa na 11 kati yao hadi sasa hawajapatikana. Kushoto kwa Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pemba Juma Khamis.
Eneo la Nugwi lina historia ya kusababisha ajali za mara kwa mara na mara ya mwisho ndiko ilitokea ajali ya meli ya MV Spice Islander iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 400 mwaka 2011.
Comments
Post a Comment