DODOMA FM 98.4 NEWS ROUND-UP: JAN 16, 2014.


WAKAZI WA MKOA WA DODOMA  WAMETAKIWA KUSHIRIKIANA KATIKA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA BADALA YA  KUTEGEMEA TAASISI MOJA PEKE YAKE.

Hayo yamesemwa na Afisa polisi Tarafa Afande George Andala akitoa ufafanuzi jinsi Dawati lilivyojipanga katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea nchini.

Akizungumza na Dodoma fm Afande  Andala amesema  wakazi Mkoani hapa wanatakiwa  kuwa kitu kimoja  na kukubaliana na dhana ya ulinzi shirikishi.Aidha  amesema kumekuwa na miradi ya watoto mashuleni inayoweza  kusaidia kupata taarifa kutoka kwa watoto huhusiana na  vitendo wanavyo fanyiwa.

Pia amesema kumekuwa na miradi ya mtandao wa familia salama na mipango ya kuongeza vituo vya redio katika kutoa elimu kuhusu masuala ya unyanya saji wa kijinsia.

 
WAKAZI WA KIJIJI CHA CHILONWAA WILAYANI CHAMWINO MKOANI DODOMA WAMEULALAMIKIA UONGOZI WA KIJIJI HICHO KWA KUTOKARABATI BARABARA NA MITARO YA MAJI MACHAFU.

Wakizungumza na Dodoma fm wakazi hao wamesema suala la miundombinu katika kijiji hicho ni tatizo kubwa  kwani ni miaka mitatu tangu barabara ziwekwe changarawe mpaka sasa hakuna kinachoendelea.

Aidha  Bi Jasmine Mkwaja amesema barabara  kijijini hapo hazijatengenezwa kwa kiwango kizuri  kwani zina makorongo na mitaro midogo midogo. Kwa upande wake Diwan wa Kata hiyo Bw  Yaled Simon amesema  barabara kwa kipindi kilichopita zilikuwa haziridhishi  lakini kwa sasa  serikali imejitahidi  na iko katika mikakati ya kuboresha zaidi.

Pia amesema kuhusu mitaro ya maji machafu serikali imewaleta mafundi na tayari wameanza zoezi la kuikarabati.

 
WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AMEWATAKA WAKAZI WA WILAYA YA KITETO MKOANI MANYARA WANAOLIMA KWENYE HIFADHI YA JAMII YA EMBOLEY MURTANGOS WARIDHIE AMRI ILIYOTOLEWA NA MAHAKAMA YA RUFAA YA KUWATAKA WAONDOKE KATIKA ENEO HILO.

Waziri Mkuu amefika kijijini hapo kwa lengo la kukagua eneo hilo kisha kuzungumza na wananchi katika viwanja vya shule ya Msingi Kibaya kufuatia taarifa za mapigano baina ya wakulima na wafugaji zilizoripotiwa siku za hivi karibuni.Baada ya  kukagua eneo husika ameteremka kwenye vitongoji vya Mtanzania na Laitimi  ambavyo vimehusika katika kupoteza baadhi ya wakazi katika mapigano hayo ambapo Kitongoji cha Mtanzania watu sita waliuawa na Laitimi  watu watatu waliuawa na kundi la wafugaji wapatao 40 -50.

Aidha amewaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kwamba kuna masuala mengi yanazunguka suala zima la Hifadhi ya Embuley Murtangos yakiwemo ya kuchelewesha usajili wa eneo husika, maamuzi wa kutengwa kwa hifadhi hiyo na kutotambulika kwa mamlaka ya sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999.

Pia Ameutaka uongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na vijiji husika ikae na kupanga upya matumizi ya ardhi na kutaka uongozi wa mkoa kushirikiana na makamishana wa polisi waliofika wilayani humo kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanakuwa salama.

 
POLISI WILAYANI KALIUA MKOANI TABORA INADAIWA KUMUUA MTU MMOJA NA KUMJERUHI MWINGINE BAADA YA WANANCHI ZAIDI YA 200 KUVAMIA KITUO KIDOGO CHA POLISI KWA LENGO LA KUMTOA MTUHUMIWA ILI KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI.

Tukio hilo limetokea baada ya wananchi wa Kijiji cha King’wangoko, Kata ya Sasu kuvamia  kituoni hapo na kutaka kumdhuru Shija Matenga, anayetuhumiwa kuiba ng’ombe watano Kasulu, Kigoma.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Peter Ouma, amesema Mkuu wa Kituo Kidogo cha King’wangoko, Sajenti Kimola alipoewa taarifa na Wakala wa Mnada kuhusu wananchi kutaka kumuua mtuhumiwa huyo.

Kutokana na hali hiyo, Sajenti Kimola alituma askari wawili wakiwa na silaha ambapo walimwokoa mtuhumiwa na kuanza kuondoka naye kitendo kilichokasirisha wananchi walioanza vurugu za kutotaka apelekwe kituoni na kupelekea  askari kupiga risasi hewani kuwatawanya.

Kwa mujibu wa Kamanda Ouma, baada ya askari kumfikisha mtuhumiwa kituoni na kumfungia mahabusu, wananchi walifuatilia na kufika kituoni alipo mtuhumiwa na kushinikiza atolewe ndipo walipofyatua risasi hewan na bahati mbaya risasi moja ilimpata John Joseph bega la kulia na kufariki papohapo.

     
HABARI ZA KIMATAIFA

NEW YORK

KAMISHNA MKUU WA HAKI ZA BINADAMU WA UMOJA WA MATAIFA, AMEZITAKA NCHI ZA KIAFRIKA KUKABILIANA NA VITENDO VYA JINAI.

Akizungumza katika Kongamano la 5 la kimataifa la nchi za Afrika, Navi Pillay amezitaka serikali za nchi za Afrika kufichua vitendo vya jinai vinavyofanywa  na kuwafikisha wahusika katika vyombo vya sheria.

Aidha amesema viongozi wa kundi la waasi wa M23 linaloungwa mkono na nchi za Rwanda na Uganda wamekiuka kwa kiwango kikubwa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hivyo viongozi wa Afrika hawapaswi kuruhusu watenda jinai wakwepe mkono wa sheria.

Pia amekumbusha baadhi ya ukatili uliofanywa na waasi wa M23 kama kuua watu kimbari, ubakaji na kutumia watoto vibaya vitani na kuongeza kuwa, watenda jinai hao wakiendeleza vitendo hivyo watahatarisha amani na utulivu wa eneo husika.

VATICAN

MAAFISA KATIKA VATICAN MAKAO MAKUU YA KANISA KATOLIKI, WANATARAJARIWA KUHOJIWA NA MAAFISA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU DHULUMA ZA KINGONO AMBAZO MAKASISI WA KANISA HILO WALIWATENDEA MAELFU YA WATOTO.

Maafisa hao walikataa ombi la awali ambapo Umoja wa Mataifa ulikuwa unataka taarifa za kina kuhusu dhuluma  hizo  wakisema kuwa visa hivyo vinapaswa kushughulikiwa na idara ya mahakama katika mataifa ambayo visa hivyo vilitokea.

Kanisa hilo limekosolewa kwa kukosa kuchukua hatua za kutosha kuhusiana na madai  hayo wakati mwaka  jana  Papa Francis alitangaza kubuni kamati yakukabiliana na visa vya dhuluma za kingono dhidi ya watoto kanisani pamoja na kutoa ushauri nasaha kwa waathiriwa.
                                         

CAIRO

MAAFISA WAKUU NCHINI MISRI WAMESIFU  IDADI KUBWA YA WATU WALIOJITOKEZA KUPIGIA KURA YA MAAMUZI KATIBA MPYA.

Afisa mmoja mkuu wa uchaguzi, Nabil Salib,ameambia vyombo vya habari kwamba idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ya maamuzi ilikuwa kubwa  kinyume na matarajio ya wengi.

Polisi wamewakamata watu 400 katika siku mbili za kwanza za kupiga kura hiyo ambao wanadaiwa kusababisha  vurugu katika shughuli hiyo.Afisaa mmoja mkuu katika wizara ya mambo ya ndani, amenukuliwa akisema huenda idadi ya wapigaji kuwa imefika asilimia 55.

 
NAIROBI

MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA UHALIFU WA KIVITA, ICC, IMEMRUHUSU NAIBU RAIS WA KENYA WILLIAM RUTO KUTOHUDHURIA BAADHI YA VIKAO VYA KESI DHIDI YAKE KATIKA MAHAKAMA HIYO.

Jaji Mkuu katika kesi yake  amesema kuwa sharti Ruto ahudhurie vikao muhimu wakati kesi yake ikiendelea, ikiwa ni pamoja na wakati  mashahidi wanapotoa ushahidi.Mwaka jana mahakama hiyo pia ilimruhusu Rais Uhuru Kenyatta kutohudhuria vikao vyote vya kesi yake.

Kenyatta na Ruto walishitakiwa kama washukiwa wakuu wa ghasia zilizozuka baada ya kuibuka utata kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 na 2008  ambapo takribani watu 1,200 waliuawa katika ghasia hizo.

Comments