WAKULIMA WA KATA YA PANDAMBILI WILAYA YA KONGWA MKOANI DODOMA WAMEIOMBA SERIKALI KUWAPA MUDA WA KUMALIZIA MSIMU WA MAVUNO YA MAZAO YAO NDIPO WAWEZE KUONDOKA KATIKA HIFADHI YA MORTANGOS.
Hayo yamefuatia baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutembelea katika eneo la hifadhi hiyo kufuatia taarifa za mapigano kati ya wakulima na wafugaji ndipo alipowataka kuondoka katika hifadhi hiyo hadi Serikali itakapowapatia ufumbuzi.
Wakizungumza na Dodoma fm wakulima hao wameomba serikali kuwapa muda kwani hawana mahali pengine pakutegemea kwa kupata chakula kwa sasa.
Aidha bwana Jonas Ngulele amesema tatizo la mgogoro wa ardhi Wilayani humo limetokana na viongozi kuto kugawa mipaka.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo Bwana Dickson Ngulele amesema kwa sasa hali ni shwari kwani watu waliokuwa wamehamia katika hifadhi hiyo wameanza kurejea nyumbani .
Pia amewaasa wakulima kuwa watulivu ili kupata suluhu na kuachana na mapigano kwani wanao athirika ni watu wasiokuwa na hatia.
WAKAZI WA KIJIJI CHA CHILONWAA WILAYANI CHAMWINO MKOANI DODOMA WAMEULALAMIKIA UONGOZI WA KIJIJI HICHO KWA KUTOKARABATI BARABARA NA MITARO YA MAJI MACHAFU.
Wakizungumza na Dodoma fm wakazi hao wamesema suala la miundombinu katika kijiji hicho ni tatizo kubwa kwani ni miaka mitatu tangu barabara ziwekwe changarawe mpaka sasa hakuna kinachoendelea.
Aidha Bi Jasmine Mkwaja amesema barabara kijijini hapo hazijatengenezwa kwa kiwango kizuri kwani zina makorongo na mitaro midogo midogo.
Kwa upande wake Diwan wa Kata hiyo Bw Yaled Simon amesema barabara kwa kipindi kilichopita zilikuwa haziridhishi lakini kwa sasa serikali imejitahidi na iko katika mikakati ya kuboresha zaidi.
Pia amesema kuhusu mitaro ya maji machafu serikali imewaleta mafundi na tayari wameanza zoezi la kuikarabati.
WAKAZI WA MKOA WA DODOMA WAMETAKIWA KUSHIRIKIANA KATIKA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA BADALA YA KUTEGEMEA TAASISI MOJA PEKE YAKE.
Hayo yamesemwa na Afisa polisi Tarafa Afande George Andala akitoa ufafanuzi jinsi Dawati lilivyojipanga katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea nchini.
Akizungumza na Dodoma fm Afande Andala amesema wakazi Mkoani hapa wanatakiwa kuwa kitu kimoja na kukubaliana na dhana ya ulinzi shirikishi.
Aidha amesema kumekuwa na miradi ya watoto mashuleni inayoweza kusaidia kupata taarifa kutoka kwa watoto huhusiana na vitendo wanavyo fanyiwa.
Pia amesema kumekuwa na miradi ya mtandao wa familia salama na mipango ya kuongeza vituo vya redio katika kutoa elimu kuhusu masuala ya unyanya saji wa kijinsia.
WAKAZI WA MBOPO NA MAENEO JIRANI WAMETANGAZA MGOGORO NA MANISPAA YA KINONDONI JIJINI DAR ES SALAAM WA KUGOMA KUPIMIWA MAENEO YAO HUKU WAKITISHIA KWENDA MAHAKAMANI ENDAPO MANISPAA HIYO ITALAZIMISHA SUALA HILO.
Akizungumza katika kikao maalumu ambacho kimewakutanisha wajumbe wa mtaa pamoja na kamati maalumu ya ufuatiliaji wa suala hilo, Mwenyekiti wa mtaa huo,Bw Abdallah Munimbo amesema hawana pingamizi na malengo yaliyowekwa na mipango miji ya Manispaa hiyo.
Aidha amesema baadhi ya wenzao wamekumbwa na tatizo la kukosa ardhi baada ya Manispaa kuchukua ardhi ya wakazi na kudai kuwa watalipa fidia huku wakiwauzia ardhi hiyo.
Bw Munimbo amesema hadi sasa wakazi wa maeneo mbalimbali ilipofanyika miradi hiyo na kusimamiwa na Manispaa ikiwemo Mabwepande wanalalamikia fidia huku wakiwa hawajapatiwa viwanja.
HABARI ZA KIMATAIFA
KIGALI
SERIKALI YA RWANDA IMELAANI VIKALI MUUNGANO WA KISIASA ULIOFANYIKA BAINA YA CHAMA CHA WAZIRI MKUU WA ZAMANI WA NCHI HIYO FAUSTIN TWAGIRAMUNGU NA MAKUNDI YA FDLR NA CHAMA CHA UPINZANI CHA PS-IMBERAKURI.
Serikali ya Rwanda imetupilia mbali mapendekezo hayo na kusema kuwa kufanya mazungumzo na watu waliofanya mauwaji ya kimbari ni kuzungumza na shetani.
Aidha Naibu muwakilishi wa Rwanda Olivya Nduhungirehe katika Umoja wa Mataifa, amesema Jumuiya ya Kimataifa imewekea vikwazo waasi wa FDLR ambao wamefanya muungano na Faustin Twagiramungu kwa madai kuwa hawawezi kufanya mazungumzo na kundi la wauaji wa Kimbari.
Muungano wa Faustin Twagiramungu na makundi ya FDLR na Chama Cha PS ulilenga kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kushinikiza serikali ya Kigali kuandaa mazungumzo ya kitaifa pamoja na maelfu ya wakimbizi kurejea nchini humo.
JUBA
MSAIDIZI WA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA ANAYESHUGHULIKIA MASWALA YA HAKI ZA BINADAM, IVAN SIMONOVIC, AMESEMA KUWA PANDE MBILI ZILIZO KWENYE MGOGORO NCHINI SUDAN KUSINI ZIMEHUSIKA KATIKA UTEKELEZAJI WA VITENDO VYA MAUAJI.
Bwana Simonovic amekuwa kwenye ziara ya maeneo mbalimbali ya Sudan Kusini ili kupata ukweli kwa ajili ya kuandaa ripoti ya Umoja wa Mataifa ambapo ameeleza kuwa ana ushahidi wa kutosha kuhusu pande hizo mbili kuwa na hatia.
Ripoti hiyo pindi itakapokuwa tayari, ataiwasilisha kwa Baraza la usalama la umoja wa mataifa ili kutathimini mauaji yaliyojitokeza katika mgogoro ulioanza mwezi Disemba mwaka jana.
Maelfu ya watu wameuawa katika mwezi mmoja uliopita katika mgogoro kati ya serikali na waasi wanaoongozwa na Makamu wa zamani wa Rais Riek Machar.
JOHANESBURG
MJUKUU WA HAYATI NELSON MANDELA, MANDLA MANDELA , AMESHITAKIWA KWA KOSA LA KUMSHAMBULIA MTU NA KUMTISHA KWA BUNDUKI.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Afrika Kusini Inadaiwa kuwa Mandla, alimshambulia mwalimu Mlamli Ngudle na hata kumtisha kwa bunduki baada ya Mwalimu huyo kuligonga gari la mmoja wa marafiki zake mwaka jana.
Mwendesha mkuu wa mashitaka amewasilisha mahakamani mashitaka mawili dhidi ya Mandla,la kwanza likiwa kumshambulia mtu na pili kumtisha kwa silaha.
Mandla ambae ni mjukuu wa kwanza wa Mandela hajasema ikiwa anakiri au kukanusha mashitaka hayo lakini wakili wake ameitaka mahakama kuahirisha kesi hiyo akitaka muda wa kutathmini ambapo imeahirishwa hadi february 24 baada ya kusikilizwa kwa muda katika mahakama ya Mhatha.
Comments
Post a Comment