TANZANIA KUSHIRIKIANA NA ALGERIA KIUCHUMI.

Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Profesa Sospeter Muhongo (picha na Urban Bulse)
Na Asteria Muhozya na Teresia Mhagama

 Tanzania kuanza kushirikiana na nchi ya Algeria katika masuala ya uchumi kupitia sekta za gesi, mafuta na umeme kutokana na mafanikio makubwa  iliyofikia nchi hiyo kupitia rasilimali hizo.


 Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu  ziara ya Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria  nchini ambaye ameongozana na ujumbe  wa wakuu  wa mashirika ya umma  ya Algeria yanayosimamia sekta za nishati na madini .

“Tanzania imekuwa ikishirikiana na Algeria hasa katika masuala ya siasa tangu enzi za vuguvugu la kupigania uhuru lakini  sasa tumeamua kushirikiana katika masuala ya kiuchumi kutokana na nchi hii kufanikiwa kupitia rasilimali za gesi,  mafuta na umeme”. Alisema Profesa Muhongo.

Aliongeza kuwa, Tanzania inaingia kwenye uchumi wa gesi na hivyo ni lazima ishirikiane na  nchi  kama  Algeria ambayo imefanya vizuri  katika sekta hii kwa takribani miaka 50 katika utafutaji na usambazaji wa nishati za gesi na mafuta na kwa sasa nchi  hiyo tayari imeshajenga mabomba mawili makubwa yanayosafirisha gesi kwenda nchi za Italia na Hispania.

“ Algeria imefanya mengi katika sekta hizi, asilimia 98 ya nchi ina umeme, vijijini umeme umesambazwa kwa asilimia 95, wana kampuni za umma  zinazosimamia sekta hii. Hivyo, tunataka kushirikiana na watu kama hawa”. Alisema Profesa Muhongo.

Alieleza kuwa nchi ya Algeria pia inasindika, inasambaza na kutengeneza mitungi ya gesi na mpaka sasa asilimia 50 ya wananchi wanatumia gesi majumbani na waliobaki wanapelekewa mitungi hivyo,  ikiwa nchi ya Tanzania inataka kufanikiwa katika sekta ya nishati ni lazima ipate uzoefu kutoka katika nchi zilizopiga hatua katika sekta hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria, Youcef Yousfi alieleza kuwa,  nchi ya Tanzania ina rasilimali nyingi,  hivyo Algeria iko tayari kushirikiana na Tanzania hasa katika suala la elimu katika masuala ya mafuta na gesi ili Tanzania iweze kuisimamia sekta ipasavyo na hivyo kunufaika na  rasilimali zake kama walivyofanikiwa wao.

Aliongeza kuwa, amefika Tanzania ili kuanza utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya mafuta , gesi, umeme na madini, yaliyosainiwa mwezi Desemba mwaka 2013 wakati Waziri wa Nishati na Madini Mhe.Profesa Sospeter Muhongo alipoitembelea nchi hiyo.

Katika ziara hii Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria ameongozana na wakuu wa mashirika  ya umma yanayosimamia sekta za nishati na madini, ambao wanakutana na wakuu wa mashirika wanaosimamia sekta hizo nchini, ili kujadiliana namna ambavyo nchi hizi zitashirikiana katika kuendeleza sekta hizo.

Comments