DAKTARI
wa Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam, Dk. Gilbert Bubelwa,
amefariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya
kuugua ugonjwa wa homa ya Dengue. Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho
jana kwa njia ya simu, Msemaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
Aminiel Algaeshi, alisema daktari huyo ambaye alilazwa hospitalini hapo
tangu Alhamisi ya wiki iliyopita, alifariki dunia juzi, saa saba usiku.
Msemaji
wa Hospitali ya Temeke, Joyce Msumba, akizungumza kwa njia ya simu,
alisema kuwa kwa sasa wamebakiwa na wagonjwa watatu ambao ni wauguzi
wawili na daktari mmoja.
Alisema hadi sasa bado hajawafahamu majina yao huku akisisitiza juhudi za makusudi zinafanyika kuwanusuru na ugonjwa huo.
Alisema
ugonjwa wa Dengue kwa Wilaya ya Temeke hasa katika hospitali hiyo
unatokana na mazingira yao na kwamba wanaendelea kumwaga dawa, ili kuua
mbu wanaoeneza ugonjwa huo.
“Ugonjwa
huu unatokea hapa hapa kutokana na mazingira, na kwamba juhudi za
makusudi zinafanyika, tayari ‘fumigation’ inafanyika kuua mbu na pia
tunahamisha wagonjwa kutoka wodi moja kwenda nyingine ili tuweze
kupuliza dawa kwa umakini,”alisema Msumba.
Alieleza
wakati ugonjwa huo unatokea, wauguzi na madaktari katika hospitali hiyo
waliacha kwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa huduma wakihofia
kupatwa na maradhi hayo.
Ugonjwa
wa Dengue umeingia jijini Dar es Salaam kwa kasi ambapo baadhi ya watu
kadhaa wameripotiwa kuugua ugonjwa huo, wakiwemo wasanii Mahsein Awadh
‘Dk. Cheni’, Rehema Chalamila ‘Ray C’, Mbunge Bahati Ally Abeid (CCM)
ambaye naye ameripotiwa kulazwa katika hospitali ya Dk. Mvungi iliyopo
Kinondoni Dar es Salaam.
Ugonjwa
huo unaoenezwa na mbu aina ya Aedes, umesambaa mkoani Dar es Salaam na
kuathiri wilaya zote tatu za Temeke, Ilala na Kinondoni.
Comments
Post a Comment