Ofisa ustawi wa jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungatuti alisema mwili wa mtoto huyo utasafirishwa leo kwenda Morogoro.
Ngungamtitu
alisema mazishi ya Nasra yatatanguliwa na ibada itakayoambatana na
utoaji wa heshima za mwisho katika Uwanja wa Jamhuri, hatua ambayo
alisema inatokana na baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi kuwa mmoja
wa watuhumiwa wa mateso yake.
Hata
hivyo, Mvungi licha ya kushiriki vikao vilivyopanga mazishi ya Nasra,
jana alisema angefurahi kama angepewa mwili wa mtoto wake ili auzike
mwenyewe badala ya kuzikwa na Serikali.
Katika
kikao cha mazishi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Al Saed, Omary Al
Saed alisema kampuni yake itatoa gharama zote za mazishi kuanzia
kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Morogoro na gharama nyingine.
Wadau
wengine ambao walitoa michango yao ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa
wa Morogoro (MRFA), Pascal Kianga na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Mateso ya Nasra
Nasra alifichwa katika boksi na mama yake mkubwa, Mariam Said mkazi wa Uwanja wa Ndege, Morogoro tangu akiwa na miezi tisa.
Alianza
kumlea mtoto huyo baada ya mdogo wake ambaye ni mama yake Nasra
kufariki dunia. Majirani wa Mariam ndiyo waliotoa taarifa za kuwepo kwa
mtoto huyo baada ya kumsikia akilia na kukohoa nyakati za usiku.
Mwanamke
huyo, Mvungi na mume wa Mariam, Mtonga Omar wamefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Morogoro kujibu mashtaka ya kula njama na
kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
Jana
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, John Laswai alisema kutokana
na kifo cha Nasra, mashtaka dhidi ya watuhumiwa yanaweza kubadilika,
lakini mabadiliko hayo yatategemea ripoti ya daktari kuhusu sababu za
kifo hicho.
Laswai
alisema taratibu za kipolisi zinafanywa kuwezesha kupatikana kwa
taarifa hiyo, ambayo itapelekwa kwa wanasheria ambao baada ya kuipitia
wanaweza kuwa na mapendekezo ya kubadili mashtaka dhidi ya watuhumiwa
hao.
Comments
Post a Comment