Treni kuchukua mizigo Bandari ya Tanga

TRENI ya mizigo ya shirika la Reli nchini (TRC), imeanza kuingia Bandari ya Tanga kwa ajili ya kubeba mizigo.

Hatua hiyo imechukuliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA),  kufuatia agizo la Makamu wa Raisi Dk Philip Mpango alilolitoa hivi karibuni, akitaka mamlaka hiyo kuhakikisha inaingia Bandari ya Tanga na kuchukua mizigo.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha amesema tayari kichwa cha treni kimeingia katika bandari hiyo kwa  ajili ya kuonesha uwezo wa kuvuta behewa mpaka tatu kwa ajili ya kupakia mzigo.

“Agizo hilo tumelifayia kazi na wiki mbili au tatu hapo nyuma nilishuhudia mimi mwenyewe kichwa cha treni kikiingia ndani ya bandari na kuanza kuonesha kitakuwa na uwezo wa kuvuta behewa mpaka tatu kwa ajili kuchukua mizigo,” amesema.

Kufuatia hatua hiyo, Mrisha amewaomba wateja wa Bandari ya Tanga ambao wanataka kusafirisha au kuchukua mizigo kutumia treni wafanye hivyo, kwa kuwa sasa treni inaingia katika bandari hiyo na kuchukua mizigo.

Comments